Skip to main content

COP27 ikielekea ukingoni Guterres amewataka wajumbe kuzingatia hasara na uharibifu

Wajumbe wakijadiliana katika siku ya mwisho ya COP27.
UNIC Tokyo/Momoko Sato
Wajumbe wakijadiliana katika siku ya mwisho ya COP27.

COP27 ikielekea ukingoni Guterres amewataka wajumbe kuzingatia hasara na uharibifu

Tabianchi na mazingira

Mkutano wa 27 wa Umoja wa Mataifa wa mabadiliko ya tabianchi utafungwa angalau siku moja baadaye kuliko ilivyotarajiwa, ofisi ya Rais wa Misri imetangaza leo Ijumaa, ikitoa wito kwa wajadili kubadili msimamo ili makubaliano yaweze kufikiwa kuhusu mambo yaliyosalia yanayohitaji mshikamano. 

"Bado nina wasiwasi na idadi ya masuala ambayo hayajakamilika, ikiwa ni pamoja na fedha za ufadhili, kukabiliana na kujenga mnepo, hasara na uharibifu na na jinsi yanavyoingiliana," Rais wa COP27, Sameh Shoukry, amewaambia wajumbe waliokutana tena katika kikao cha baraza la kimataifa la Sharm el-Sheik. 

Bwana Shoukry ametoa wito kwa wahusika kufanya kazi kwa pamoja haraka ili kutatua maswala ambayo hayajakamilika haraka iwezekanavyo na akaongeza kuwa anatumai kukamilisha mkutano huo kufikia kesho Jumamosi. 

Mapema leo asubuhi, katika juhudi za kuchochea mazungumzo hayo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alikutana kando na wanachama wa Muungano wa Ulaya na kundi la nchi 77 na China ambalo linajumuisha karibu nchi zote zinazoendelea. 

Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa pia amekutana na mjumbe maalum wa mabadiliko ya tabianchi wa China, Xie Zhenhua, na kuendelea na mashauriano ya kina na pande kadhaa. 

"Mazungumzo yanapofikia tamati, Katibu Mkuu anazitaka pande husika kuwa na malengo ya juu zaidi ya hasara na uharibifu na kupunguza uzalishaji wa hewa chafuzi," amesema Bwana Guterres katika barua aliyoitoa huko Sharm el-Sheikh kupitia msemaji wake. 

Nakeeyat Dramani Sam, mwanaharakati mwenye umri wa miaka kumi kutoka Ghana, akihutubia mkutano wa COP27.
UNIC Tokyo/Momoko Sato
Nakeeyat Dramani Sam, mwanaharakati mwenye umri wa miaka kumi kutoka Ghana, akihutubia mkutano wa COP27.

Msichana aliyekemea wajumbe 

"Je, kuna wajumbe wengine ambao wanataka kutoa tamko?" Rais Shoukry aliuliza katika kile kinachojulikana kama kikao cha uhesabuji hisa, ambapo mchakato wa hatua zinazopigwa unafanyika kila siku. 

Ujumbe wa Ghana uliomba nafasi hiyo, na ukapitisha kipaza sauti kwa Nakeeyat Dramani Sam mtoto mwenye umri wa miaka 10. 

Mwanaharakati huyo mchanga alianza kuwakemea wajumbe kwa kuonekana kutofaulu kulichukulia janga la mabadiliko ya tabianchi kwa uzito, wangechukua hatua haraka kukomesha ongezeko la joto duniani ikiwa wangekuwa na umri kama wake, amesema binti huyo. 

“Kama ninyi nyote mngekuwa vijana kama mimi, si mngekuwa tayari mmekubali kufanya kile kinachohitajika ili kuokoa sayari yetu? Je, tuwaache vijana wachukue madaraka? Labda ni wajumbe wa vijana pekee ndio wanapaswa kuwa kwenye COP ijayo”, amesema mtoto huyo, huku akiamsha wajumbe wote waliohudhuria kumpigia shangwe. 

Binti Dramani Sam amewataka watu wazima kuwa na moyo na kufanya hesabu, akimaanisha sayansi inayoonyesha uzito wa mabadiliko ya tabianchi katika siku zijazo. 

"Ni matumaini yangu ya dhati kwamba COP27 itachukua hatua kwa ajili yetu. Nina uhakika hakuna anayetaka kutusaliti,” ameongeza binti huyo. 

Mwanaharakati huyo wa watoto pia ameomba mataifa kuchimba mifukoni mwao na kutoa pesa kwa wale wanaoteseka zaidi. 

 Ameongeza kuwa "Baadhi ya jamii katika nchi yangu zinalipa gharama kubwa tangu sayari yetu ilipoanza kuchomwa moto na baadhi ya watu. Hii inaweka swali rahisi kwenye jedwali. Unaweza kutulipa lini? Kwa sababu malipo yamechelewa.”. 

Hali ilivyo sasa katika mkutano huo 

Maamuzi ya mkutano huo yalichapishwa usiku wa kuamkia Alhamisi. Hati hiyo inathibitisha tena leongo la kuhakikisha joto linasalia nyuzijoto 1.5C ili kukabiliana na ongezeko la joto duniani na inakaribisha ripoti za jopo la Serikali mbalimbali kuhusu mabadiliko ya tabianchi (IPCC). 

Pia inataka kupunguzwa kwa kina, na haraka kwa utoaji wa hewa chafuzi na vile vile kuongeza kasi ya mabadiliko ya kuingia katika nishati safi katika miaka hii ya ya 2020. 

Maandishi ya maamuzi hayo pia yanaweka lugha ya COP26 kwenye "kupunguza nguvu ya makaa ya mawe na kutoa wito kwa wanachama kurekebisha ruzuku ya mafuta kisukuku na kuhimiza mipango mipya ya kitaifa ya hatua za mabadiliko ya tabianchi (NDC's) ifikapo 2023.” 

Rasimu ya matokeo inakaribisha kipengee cha ajenda ya hasara na uharibifu, lakini haitaji uundaji wa kituo au ufadhili. 

Pia leo Ijumaa, Muungano wa Ulaya umewasilisha pendekezo rasmi la kuunda hazina ya hasara na uharibifu, na kuamsha matumaini kwa kile ambacho baadhi ya wajumbe kutoka nchi zinazoendelea wamesema kinaweza kuwa mafanikio. 

Mashirika ya kidini nayo  hayakuwa nyuma huko COP27 yakitaka mafuta ya kisukuku yasalie ardhini kwani yanachangia hewa ya ukaa
UN News/Laura Quinones
Mashirika ya kidini nayo hayakuwa nyuma huko COP27 yakitaka mafuta ya kisukuku yasalie ardhini kwani yanachangia hewa ya ukaa

NGOs wadhihirisha hisia zao 

Wakati huo huo, mwitikio wa wanaharakati kutoka mashirika ya kiraia kwa rasimu ya hivi karibuni na mazungumzo hayo kwenda polepole umedhihirika kupitia mikutano ya waandishi wa habari na maandamano madogo katika eneo lote la COP27. 

COP27 kweli iko kwenye njiapanda amesema Catherine Abreu, kutoka shirika lisilo la kiserikali NGO la Destination Zero akiwaambia waandishi wa habari. 

Kwa upande wake mkutano huu wa COP una fursa ya kuwa mfano kwa kuweka kipaumbele cha juu katika suala la hasara na uharibifu na haki ya kuhamia kwenye nishati jadidifu na kuachana na matumizi ya mafuta kisukuku. 

“Urais wa Misri na nchi nyingine zinazohusika katika mazungumzo haya zina chaguo. Je, tunatoka kwenye hii COP tukisema tuna kitu dhahiri cha kuleta nyumbani kwa jamii zetu?  Au tunaondoka katika COP hii mikono mitupu na ahadi hewa ambazo tumekuwa tukitoka nazo katika mikutano mingine ya COP katika miongo mitatu iliyopita ,? Ameongeza akimiza ahadi ya kudhibiti ongezeko la joto duniani lisizidi nyuzi joto 1.5C kwa kusongesha juhudi za kuachana na mafuta kisukuku na kushughulikia athari zake kote duniani. 

Chiara Martinelly, mkurugenzi wa mtandao wa Climate Action akizungumzia suala la hasara na uharibifu, amesema kuwa "Fedha zipo. Ni vyema kusikia pendekezo la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuchimba suluhisho la vyanzo vya ubunifu vya ufadhili," amesema, akimaanisha hotuba ya ufunguzi wa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo alisema kuwa kampuni za mafuta zinaweza kutozwa ushuru ili kulipa nchi fidia za uharibifu unaosababishwa na mabadiliko ya tabianchi duniani kote.