Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio lingine Kabul, UN yapaza sauti

Taswira ya Kabul, mji mkuu wa Afghanistan. (Picha:UNAMA/Fardin Waezi)

Shambulio lingine Kabul, UN yapaza sauti

Amani na Usalama

Umoja wa Mataifa umelaani vikali shambulio lililofanywa na wapiganaji wa Talibani kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul na kusababisha vifo vya watu 48 huku wengine wengi 67 wakijeruhiwa.

Katibu Mkuu Antonio Guterres ametuma salamu za rambarambi kwa wale ambao jamaa na ndugu zao wamepoteza maisha kwenye shambulio hilo la jana.

Vyombo vya  habari vinasema kuwa idadi kubwa ya waliopoteza maisha ni watoto walio na umri wa chini ya miaka 18.

Yaelezwa kuwa mshambuliaji wa kujilipua aliingia darasani wakati wanafunzi wanasoma na kulipua bomu alilokuwa amejifunga kiunoni.

Wanafunzi hao waliokuwa darasani walikuwa wanapata mafunzo ya ziada wakijiandaa na mtihani wa kujiunga na Chuo Kikuu.

Katibu Mkuu amesema kulenga raia hususan watoto ni jambo lisilokubalika na ametakia ahueni ya haraka majeruhi huku akisisitiza wahusika wawajibishwe.

Nalo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limetoa taarifa kulaani kitendo hicho likisisitiza kuwa wahusika lazima wafikishwe mbele ya sheria.

Shambulio hili la Kabul linakuja siku chache baada ya mashambulio mengine jimboni Ghazni ambayo nayo yalisababisha vifo na majeruhi.