Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Acheni raia wa Ghazni wapate matibabu-UN

Mazishi ya raia waliouawa kwenye shambulio la kujitoa muhanga mjini Kabul , Afghanistan Juni 2018. Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo , UNAMA umeripoti kuwa idadi ya raia waliouawa na pande hasimu nchini humo katika nusu ya kwanza ya 2018
Fardin Waezi/UNAMA
Mazishi ya raia waliouawa kwenye shambulio la kujitoa muhanga mjini Kabul , Afghanistan Juni 2018. Mpango wa Umoja wa Mataifa nchini humo , UNAMA umeripoti kuwa idadi ya raia waliouawa na pande hasimu nchini humo katika nusu ya kwanza ya 2018

Acheni raia wa Ghazni wapate matibabu-UN

Afya

Pande zote husika katika mgogoro nchini Afghanistan zimetakiwa kuheshimu sheria za kimataifa za kibinamu na hivyo zilinde maisha ya raia, haki za binadamu pamoja na miundombinu ya raia.

Hayo yametamkwa leo mjini Kabul, mji mkuu wa Afghanistan, na kaimu mratibu wa masuala ya kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini humo ,Dkt Rik Peeperkorn kufuatia eneo la Ghazni nchini humo kugeuzwa uwanja wa mapambano tangu Ijumaa asubuhi.

Amesema wamepokea ripoti ya vifo na majeruhi miongoni mwa raia na watu wakihaha kufikia maeneo salama nje ya mji huo.

Halikadhalika amesema dawa katika hospitali kuu mjini Ghazni zimepungua na watu wanashindwa kufikisha majeruhi kwa ajili ya matibabu kwasababu bararaba kuu za kutoka kaskazini na kusini mwa mji huo zinagombaniwa kati ya pande kinzani na hivyo si salama kwa watu kusafiri.

Vyanzo vya habari vinasema kuwa wapiganaji wa kitaliban wanadhibiti maeneo ya mashambani ya mkoa huo  na wanapigana na vikosi vya serikali kutaka kudhibiti mji wa Ghazni ambao ni wa saba kwa ukubwa nchini humo.

Dkt. Peeperkorn amesema kuwa wakazi wa mji wa Ghazni wameshuhudia mji wao ukigeuzwa kuwa uwanja wa mapambano tangu Ijumaa asubuhi na mapigano yanaripotiwa kuendelea hadi sasa.

 Taarifa  mbalimbali  kutoka mji wa Ghazni zasema kuwa familia nyingi zimejificha majumbani mwao na ni vigumu kuondoka. Mji wenye watu 270,000 hauna mawasiliano yoyote  muhimu, wala umeme huku maji na chakula vinazidikupungua.

Vyanzo kadhaa vya habari vinaeleza mpaka sasa raia  20 wameuawa ilhali  takriban askari 100 wamepoteza maisha yao katika mapigano hayo kati ya vikosi vya serikali na wapiganaji wa kitalibani.

 Ni kwa mantiki hiyo kaimu  huyo mratibu wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistani ametoa wito kwa pande hizo zihakikishe kuwa watu wanaweza kupata huduma za matibabu na pia  vituo vya afya pamoja na wafanyakazi wake wanalindwa.