Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shinikizo la huduma za afya kwa wakimbizi wa Rohingya laongezeka:WHO

Mtoto wa kabila la Rohingya baada ya kupatiwa matibabu dhidi ya ugonjwa wa donkakoo huko Cox's Bazar nchini Bangladesh. (Picha:IOM)

Shinikizo la huduma za afya kwa wakimbizi wa Rohingya laongezeka:WHO

Wahamiaji na Wakimbizi

Kuendelea kushika kasi kwa msimu wa pepo kali na mvua za monsoon kumeongeza shinikizo la mahitaji ya kiafya kwamaelfuya wakimbiz wa Rohingya walioanza kumiminika nchini Bangladesh kwa wingi yapata miezi 10 iliyopita.

Kwa mujibu wa shirika la afya duniani WHO, mvua kubwa zinazoendelea kunyesha zimeshababisha mafuriko kambini Cox’s Bazar na kuongeza hatari ya magonjwa yatokanayo na maji kama kuhara na homa ya ini au Hepataitis, lakini pia magonjwa yanayoenezwa na wadudu kama vile malaria, homa ya Dengue na chikungunya. Christian Lindmeier ni msemaji wa WHO Geneva

 “Sekta ya afya ambayo inaupungufu mkubwa wa ufadhili inasuasua kukidhi mahitaji ya kiafya kwa watu hawa wasiojiweza. Hadi sasa sekta hiyo imepokea asilimia 12 tu ya dola milioni 113.1 inazohitaji kwa ajili ya mkakati wa pamoja wa mwaka 2018.”

Ameongeza kuwa kati ya fedha hizo WHO imeomba dola milioni 16.5 kwa mwaka  huu wa 2018. Takribani wakimbizi wa Rohingya 700,000 wamevuka mpaka na kuingia Bangladesh kutoka jimbo la Rakhine nchini Myanmar tangu 25 Agosti 2017, na karibu watu milioni 1.3 wanapatiwa msaada wa kibinadamu wakiwemo wakimbizi wapya na jamii za wenyeji zilizowapokea.