Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baba msikimbie familia mtoto mlemavu wa ngozi anapozaliwa- Mawunyo

Mawunyo Yakor-Dagbah, (kushoto) Makamu Rais wa Shirikisho la Vyama vya watu wenye ulemavu nchini Ghana, GDF akihojiwa na Assumpta Massoi wa UN News jijini New York, Marekani.
UN News/Ben Malor
Mawunyo Yakor-Dagbah, (kushoto) Makamu Rais wa Shirikisho la Vyama vya watu wenye ulemavu nchini Ghana, GDF akihojiwa na Assumpta Massoi wa UN News jijini New York, Marekani.

Baba msikimbie familia mtoto mlemavu wa ngozi anapozaliwa- Mawunyo

Haki za binadamu

Pale familia moja inapokuwa na watoto watatu wenye ulemavu wa ngozi katika jamii ambamo kwayo bado kuna fikra potofu. Je hali inakuwa vipi?

Ilikuwa vigumu sana kwa wazazi wetu kutukuza watoto watatu wenye ulemavu wa ngozi. Hiyo ni kauli ya  Mawuyo Yakor-Dagbah, [YAKO DAGBA], raia wa Ghana mwenye ulemavu wa Ngozi.

Mawunyo ambaye sasa ni Makamu wa Rais wa shirikisho la vyama vya watu wenye ulemavu nchini humo, akisimulia yale waliyopitia yeye na wadogo zake wawili ambao wote wana ulemavu wa ngozi amesema..

Sauti ya Mawunyo Yakor-Dagbah

“Ilikuwa changamoto kubwa, vile wanakutazama na kukuimbia, unajua wakati mwingine watoto wanaweza kuwa na ukatili. Unapita na wanaimba nyimbo kwamba wewe ni wa ajabu mbele yao, basi  unajisikia vibaya kwamba yaani mimi si binadamu.”

Hata hivyo akifika nyumbani…

Sauti ya Mawunyo Yakor-Dagbah

 “Mama yangu atasema usiwajali, wewe uko sawa na wengine, na unafanya vizuri shuleni kuliko wengine. Kwa hiyo alikuwa anasema hivyo ili kukutia moyo uendelee kujikita shuleni.”

 Mawunyo ambaye jina lake linamaanisha Mungu ni mwema akawa na ujumbe kwa wazazi hususan akina baba wanaokimbia familia zao pindi mtoto mwenye ulemavu anapozaliwa.

 Sauti ya Mawunyo Yakor-Dagbah

 “Tafadhali sote tuna uwezo. Tafadhali salía nyumbani na hakikisha unampa mtoto msaada wowote hata kitu kidogo ili ajihisi wa kawaida na pindi atakapokua mkubwa atakabiliana na changamoto zote.”

 Hivi sasa Mawunyo ni mkaguzi wa hesabu mwandamizi katika ofisi ya taifa ya ukaguzi wa hesabu nchini Ghana.