Tushikamane tusongeshe haki za watu wenye ulemavu wa ngozi- UN
Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kuelimisha jamii kuhusu watu wenye ulemavu wa ngozi au Albino, Umoja wa Mataifa unapigia chepuo zaidi harakati za kulinda kundi hilo ili liweze kuishi kwa amani bila woga.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres katika ujumbe wake wa siku hii ametaja hatua hizo kuwa ni pamoja na Mpango wa utekelezaji wa Afrika kuhusu Albino uliopitishwa na kamisheni ya haki za binadamu ya Afrika na bunge la Afrika.
Hata hivyo amesema hatua zaidi zapaswa kuchukuliwa duniani kote ili kuongeza uelewa wa madhila yanayokumba wanawake na wanaume wenye ulemavu huo wa ngozi ambao hupata watu bila kujali jinsia, rangi au kabila.

Katibu Mkuu amesema ajenda 2030 ya maendeleo endelevu imetoa ahadi ya kutokumwacha nyuma mtu yeyote.
Kwa mantiki hiyo ametaka siku ya leo iwe fursa ya kutangaza mshikamano na watu wote duniani wenye ulemavu wa ngozi na kushirikiana kusongesha haki zao ili waweze kuishi kwa amani bila ubaguzi, wahamasike na wafurahie kikamilifu haki za binadamu.