Visa vya malaria vinaongeza mzigo wa kukabiliana na Ebola, DRC

28 Novemba 2018

Kampeni ya kutoa dawa dhidi ya ugonjwa wa Malaria imezinduliwa leo jimbo la Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC kufuatia ongezeko la visa vya ugonjwa huo  kwenye eneo hilo ambako tayari wahudumu wa afya wanahaha kukabiliana na mlipuko wa Ebola.

Kampeni hiyo ya siku nne  inayohusisha ugawaji wa dawa na vyandarua vya kuzuia mbu inalenga watu takriban 450,000.

Kampeni hiyo inaendeshwa na programu ya taifa ya kukabiliana na malaria, DRC kwa msaada wa shirika la afya ulimwenguni, WHO, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, mfuko wa kimataifa na programu ya rais wa Marekani ya kukabiliana na Malaria.

 Akizungumzia ongezeko la visa vya Malaria, mwaklishi wa WHO nchini DRC, Dkt, Yokouide Allarangar amesema, “kudhibiti malaria ni muhimu katika maeneo kama Kivu Kaskazini kwa sababu unasababisha vifo hususan kwa watoto.” 

Ameongeza kuwa kampeni hiyo itasaidia kuondoa shinikizo kwa mfumo wa afya ambao kwa sasa unalenga kulinda watu dhidi ya Ebola.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na WHO ongezeko la wagonjwa wa Malaria linaongeza mzigo kwa watoa huduma wa Ebola ambapo visa vingi vilivyoshukiwa kuwa ni Ebola vimepatikana kuwa ni malaria kwani dalili za kwanza za magonjwa yote zinafanana, “huku asilimia 50 ya watu waliochunguzwa kutibiwa Ebola wamepatikana kuwa na Malaria.”

“Lengo la kampeni ni kusambaza vyandarua ambavyo vitazuia kusambaa kwa malaria na changamoto zake na hivyo kuokoa maisha na pili ni kutibu watu ambao tayari wamepatikana kuwa na malaria ili kupunguza mzigo kwa wanaokabiliana na Ebola,” imesema WHO.

Kwa mujibu wa WHO, DRC ni nchi ya pili duniani kwa kuwa na visa vingi vya Malaria ambapo nchi inayoshika nafasi ya kwanza ni Nigeria.

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2017, DRC ilibeba asilimia 11 ya visa milioni 219 vya malaria duniani ambapo vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vilikuwa 435, 000.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud