"Tunaushukuru Umoja wa Mataifa kwa kujadili moja ya matatizo yetu makubwa": Tanzania
Mjadala wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kikao cha 73 unaendelea mjini New York Marekani na leo , unajikita katika afya hususan jinsi ya kupambana na ugonjwa wa kifua au TB kikuu kote duniani.
Shirika la afya ulimwenguni WHO, wataalamu wa afya, watafiti na mawaziri wa afya na wawakilishi wa sekta za afya kutoka nchi wanachama wanahudhuria mjadala huo. Tanzania inawakilishwa na Ummy Mwalimu ambaye ni waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia watoto na wazee.
Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa amesema moja ya mambo yaliyoifurahisha Tanzania katika mjadala wa Baraza Kuu mwaka huu ni kuamua kujadili Ugonjwa wa kifua kikuu.
“Tunashukuru kuona umoja wa mataifa unajadili ugonjwa wa kifua kikuu kwasababu Tanzania ni moja ya nchi 30 zenye idadi kubwa ya wagonjwa wa kifua kikuu”
Ni Waziri wa Afya nchini Tanzania akieleza hali ya Ugonjwa wa kifua kikuu ilivyo nchini mwake.
Waziri Ummy, pia anasema pamoja na Tanzania kujitahidi katika matibabu, changamoto kubwa ambayo nchi yake Bado inakabiliana nayo ni kuwaibua wagonjwa wapya wa Kifua kikuu. Amesema inakadiriwa kuwa katika watu 100 wenye Ugonjwa wa kifua kikuu nchini Tanzania, 56 kati yao hawajafikiwa ili kuingizwa katika utaratibu wa matibabu.
Je! Wana wana mkakati gani kuwatambua wagonjwa wapya na kuwafikishia matibabu?
“Sasa hivi, mtu yeyote ambaye ataenda katika kituo cha kupata huduma za afya tutamuhisi kama mgonjwa wa kifua kikuu. Kwa hiyo ataulizwa vidokezo kama kumi hivi ambavyo vitatusaidia kumweka kwenye nafasi ya pili.”
Amesema tiba za jadi ni changamoto wanakabiliana nayo kwa kutoa elimu
“Tumewapa mafunzo waganga wa kienyeji na tumewaeleza pale ambapo mtu amekuja kwako ana kifua kikuu umempa dawa zako, siku ya kwanza ya pili hapati nafuu yoyote, mpe rufaa”
Aidha Tanzania kwa kushirikiana na wakfu wa kimataifa wa kupambana na Ukimwi, Malaria na Kifua Kikuu Global Fund, wamenunua mashine mpya za kupima ambazo hutoa majibu ndani ya muda mfupi wa saa mbili.
Ripoti ya shirika la afya ulimwenguni WHO iliyotolewa katikati ya mwezi huu kuhusu hali ya ugonjwa wa TB duniani, inasema idadi ya watu waliougua kifua kikuu au kufariki dunia mwaka jana ilikuwa ni ndogo ingawa bado mataifa mengi hayachukui hatua za kutosha kuweza kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka wa 2030.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa licha ya juhudi zilizoweza kuzuia vifo vya watu milioni 54 duniani kote kutokana na kifua kikuu tangu mwaka wa 2000, bado TB inasalia kuwa ugonjwa hatari wa kuambukiza.