Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Global Fund yasaka dola bilioni 14 kupambana na TB, UKIMWI na malaria

Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa
Photo: The Global Fund/John Rae
Mashine kwa udhamini wa Global Fund ili kupambana na VVU, Kifua Kikuu na Malaria inawasaidia maafisa wa afya wa gereza la Pollsmoor Afrika Kusini kuwapima na kuwatibu wafungwa

Global Fund yasaka dola bilioni 14 kupambana na TB, UKIMWI na malaria

Afya

Mfuko wa kimataifa wa kusaidia mapambano dhidi ya virusi vya HIV, kifua kikuu au TB na malaria (Global Fund) umesema unahitaji kuchangisha dola bilioni 14 ili kuongeza kasi ya vita dhidi ya magonjwa hayo katika miaka mitatu ijayo.

Katika mkutano maalum wa sita wa uchangishaji fedha unulioanza jana mjini Lyon Ufaransa  ambao unakunja jamvi hii leo rais wa Global Funds Peter Sands amesema amesema fedha hizo zitasaidia kuokoa maisha ya watu milioni 16, kuepusha maambukizi mapya milioni 234 na kuisaidia dunia kurejea kwenye msitari wa kupambana kukomesha magonjwa hayo matatu hatari.

Mbali ya dola hizo bilioni 14 zinazohitajika Global Fund imetoa wito kwa sekta binafsi kuchangisha takribani dola bilioni moja ili kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya magonjwa hayo.

Akizungumza kwenye mkutano huo mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani Dkt. Tedross Adhamon Ghebreyesus amesisitiza kuwa “kuongeza nguvu ya kupambana na maradhi hayo isionekane kama ni chaguo , lakini utimizaji wa ahadi zetu , wakati huu unatupa fursa ya kuchukua hatua Madhubuti ya kufikia lengo la maendeleo endelevu namba 3 la afya na ustawi bora kwa wote. Hatuna muda wa kupoteza na kunatoa wito kwa dunia kuongeza kasi ya hatua sasa.”

Naye Rais wa Global Fund Peter Sands amesema, “Hadi sasa tumefanya vyema katika kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na magonjwa haya matatu kuliko kupunguza idadi ya visa na maambukizi, tumeokoa Maisha ya watu milioni 27, mafanikio makubwa , lakini hatimaye ili kukomesha maradhi hayo na kuokoa Maisha ya mamilioni ni lazima tuongeze kasi ya kupunguza maambukizi mapya.”

Ameongeza kuwa fedha hizo dola bilioni 14 zitatumika katika miaka mitatu ijayo kuanzia 2020 hadi 2023 zikijikita Zaidi katika kukomesha maambukizi mapya, kuhakikisha wagonjwa wanapata huduma zinazostahili na kuzisaidia nchi kuwa na mkakati wa kutimiza lengo la maendeleo endelevu namba 3.