Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ebola yaibuka tena DRC

Juhudi za kukabiliana na Ebola katika kituo cha huduma za afya nchini DRC. Picha: WHO

Ebola yaibuka tena DRC

Afya

Ebola yabisha tena hodi DRC, ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu mlipuko mwingine utokee nchini humo kipindi kama hiki na kudhibitiwa baada ya miezi mitatu.

Serikali ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo, DRC hii leo imetangaza mlipuko wa Ebola huko Bikoro jimbo la Equateur.

Tangazo hilo linafuatia maabara ya kitaifa ya kitabibu huko Kinshasa, kuthibitisha visa viwili kati ya sampuli tano zilizowasilishwa kwa uchunguzi.

Shirika la afya ulimwenguni, WHO tayari limethibitisha kupokea kwa taarifa za mlipuko huo kutoka serikali ya DRC ambapo hivi sasa sampuli zaidi zinawasilishwa kwenye maabara kwa ajili  ya uchunguzi.

Naibu Mkurugenzi WHO Peter Salama amesema hivi sasa wanashirikiana na serikali na wadau wengine ili ikuimarisha operesheni za kuzuia kuenea kwa Ebola kwenye jimbo hilo lililo kaskazini-magharibi mwa nchi.

Wakati wa mlipuko wa Ebola huko DRC mwaka 2014,  maafisa waandamizi wa UN na serikali ya DRC walitathmini kwa pamoja hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.
MONUSCO/Jesus Nzambi
Wakati wa mlipuko wa Ebola huko DRC mwaka 2014, maafisa waandamizi wa UN na serikali ya DRC walitathmini kwa pamoja hatua za kukabiliana na ugonjwa huo.

Amesema wanatumia  mfumo wa udhibiti waliotumia wakati wa mlipuko wa Ebola mwaka jana, mfumo ambao uliwezi kudhibiti na kutokomeza mlipuko ndani ya miezi mitatu.

Tayari timu ya kwanza kutoka wizara ya afya ya DRC, WHO na wadau wakiwemo madaktari wasio na mipaka, MSF wamekwenda Bikoro ili kuimarisha uchunguzi na udhibiti wa Ebola.

Katika kipindi cha wiki tano zilizopita kumeripotiwa homa inayohusisha watu kutokwa na damu kwenye eneo hilo la Bikoro ambapo watu 17 wamefariki dunia.

Huu ni mlipuko wa tisa nchini DRC tangu mwaka 1976, ambapo mlipuko wa mwaka jana ulitokea katika jimbo la Bas-Ulele mwezi Mei na kutokomezwa mwezi Julai.