Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hakuna haja ya kutangaza udharura wa kiafya duniani kutokana na Ebola DRC

Wahudumu wa afya wakijiandaa kushughulikia wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa wa ebola hospitali ya Bikoro nchini DRC
UNICEF/Mark Naftalin
Wahudumu wa afya wakijiandaa kushughulikia wanaoshukiwa kuwa na ugonjwa wa ebola hospitali ya Bikoro nchini DRC

Hakuna haja ya kutangaza udharura wa kiafya duniani kutokana na Ebola DRC

Afya

Hii leo WHO ilikuwa na kikao cha kamati ya dharura kuangazia iwapo mlipuko wa Ebola  huko DRC unasababisha udharura katika afya ya umma ulimwenguni au la. Wataalamu wamekutana na kumshauri Mkurugenzi Mkuu naye ametangaza uamuzi wake.

 Mlipuko wa Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC si tishio la afya ya umma duniani kwa sasa.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya ulimwenguni, WHO Dkt. Tedros Ghebreyeus ametangaza uamuzi huo leo baada ya kikao cha kamati ya dharura ya wataalamu huko Geneva, Uswisi.

Pamoja na kutotangaza hali hiyo, kamati imeshauri pia kutokuwekwa kwa vikwazo vya safari dhidi ya DRC kwa kuwa hatua zilizochukuliwa na serikali na wadau wake kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo zinatia matumaini.

Kabla ya kutoa uamuzi, wataalamu walisikiliza ripoti za udhibiti wa Ebola kutoka kwa wadau wakiwemo wawakilishi wa serikali ya DR Congo ambao wameelezea hatua zinazoendelea kuchukuliwa hivi sasa kutibu na kukinga ugonjwa huo na changamoto zilizopo.

Kwa upande wake wajumbe wa kamati hiyo ya dharura walimpatia mkurugenzi mkuu wa WHO tathmini ya hali halisi ya mlipuko ikiwemo idadi ya visa shukiwa ambavyo hadi sasa ni 45 na vifo ni 25.

Image
Mkurugenzi mpya mteule wa WHO,Dr Tedros Adhanom Ghebreyesus.(Picha:UM/Daniel Johnson)

Halikadhalika walieleza kuwa nchi 9 jirani ambazo ni pamoja na Congo-Brazzaville na  Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR zimeshauriwa kuwa makini kujikinga na ugonjwa huo huku zikipatiwa vifaa na wahudumu wa kusaidia kujikinga.

Baada ya kupokea taarifa hizo, kamati ilibaini changamoto kama vile uwezekano wa ugonjwa kuenea kwa kuwa mji wa Mbandaka ambako kumeripotiwa pia Ebola, uko kando mwa mto Congo ambao ni mpakani na huhusisha watu kutoka pande mbalimbali.

Halikadhalika changamoto ya vifaa na uwezo wa kupima watu na kubaini.

Hata hivyo kamati hiyo ilibaini kuwa serikali ya DRC kwa kushirikiana na WHO na wadau wengine ilichukua hatua haraka kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

 

(Picha:UNNewsKiswahili/Assumpta Massoi)
Ebola!

Halikadhalika usambazaji wa chanjo dhidi ya Ebola unatoa matumaini zaidi ya udhibiti wa kuenea kwa ugonjwa huo.

Kwa mantiki hiyo wataalamu wameona kuwa kwa mazingira ya sasa hakuna haja ya kutangaza kuwa mlipuko huo unaleta udharura katika kushughulikia afya ya umma duniani.

Hata hivyo wamesihi serikali ya DRC, WHO na wadau waendelee kuwa makini katika udhibiti wa ugonjwa huo, huku wakiomba jamii ya kimataifa iunge mkono.

WHO imesema kamati hiyo itaitishwa tena iwapo kutakuwepo na taarifa za kuenea zaidi kwa ugonjwa huo.

Hii ni mara ya kwanza kwa kamati hiyo ya dharura ya kitaalamu kuundwa mwaka huu.

Kamati hizi huundwa pindi mlipuko wa magonjwa unapoonekana kutishia afya ya umma. Mathalani wakati wa mlipuko wa Zika huko Amerika ya Kusini mwaka 2016 pamoja na mlipuko wa Ebola huko Libera kuanzia mwaka 2014 hadi 2016 uliosababisha vifo vya watu wapatao 11,300.