Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mlipuko wa virusi vya Ebola wathibitishwa DRC-WHO

Mlipuko wa virusi vya Ebola wathibitishwa DRC-WHO

Waziri wa afya nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC Dr Oly Ilunga Kalenga, Ijumaa ameliarifu shirika la afya duniani WHO kuhusu mlipuko wa virusi vya homa ya Ebola katika eneo la Aketi jimbo la,Bas-Uélé zaidi ya kilometa 1300 kutoka mji mkuu Kinshasa .

Taarifa hizo ni kufuatia kuthibitishwa kwa Ebola na kituo cha kitaifa cha utafiti wa kitabibu (INRB) na maabara ya taifa baada ya sampuli za damu za watu watano waliokuwa wakishukiwa kuwa na Ebola kupimwa na mmoja kukutwa na virusi hivyo.

Waziri huyo katika barua aliyoiwasilisha kwa mwakilishi wa WHO nchini DRC ameomba pia usaidizi wa kuimarisha uwezo wa kukabiliana na mlipuko huo. Tangu Aprili 22 mwaka huu visa 9 vinavyoshukiwa kuwa Ebola vimeripotiwa ikiwemo vifo vitatu katika kituo cha afya cha Likati .

Hivi sasa ofisi ya WHO DRC inashirikiana na serikali, mamlaka za majimbo, ofisi ya kanda ya Afrika ya WHO, makao makuu ya WHO Geneva na wadau wengine ili kupeleka wahudumu wa afya na vifaa vya kinga kuweza kudhibiti mlipuko huo, timu ya uchunguzi imeshatumwa na inatarajiwa kuwasili eneo husika siku chache zijazo.