Huduma ya afya bila malipo DRC ni ya muhimu lakini ina changamoto nyingi-UNICEF

15 Novemba 2018

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, huduma ya utoaji wa matibabu bure kwenye maeneo yaliyokumbwa na mlipuko wa Ebola, haujawa na matokeo chanya kama ilivyotarajiwa.

Shirika la kuhudumia watoto duniani, UNICEF limesema  hayo katika makala iliyoandikwa na mwandishi wa habari kijana na kuchapishwa kwenye wavuti wa shirika hilo.

Taarifa hiyo inasema ili kupambana na Ebola, serikali ya DRC ilitangaza matibabu ya bure katika maeneo yote yaliyokumbwa na ugonjwa huo ambapo huduma hiyo ilionekana kuwa jambo jema kwa kuzingatia kuwa idadi kubwa ya wakazi wa eneo hilo hawana kipato cha kutosha kulipia matibabu.

“Hata hivyo, katika eneo la Bikoro, eneo la huduma ya afya lililoko kama mia moja kutoka Mbandaka, huduma ya afya ya bure imekuwa na matokeo mabaya ambayo hayakutegemewa. Tangu huduma ya afya ilipoanza kutolewa bila malipo, inachukua saa lukuki kwa mgonjwa kuonwa na mmoja wa madaktari katika hospitali ya rufaa,” imesem taarifa hiyo ikiongeza kuwa mgonjwa anaweza kufika hospitali saa mbili asubuhi akiwa na mtoto anayeumwa sana lakini hatatibiwa mpaka mchana bila kujali anaumwa kwa kiasi gani.

Mwandishi wa taarifa hiyo anasema alipozungumza na watoa huduma za afya aligundua kuwa tangu huduma ya afya bila malipo ilipoanza kutolewa, wahudumu hao hawapokei tena marupurupu au motisha. “Marupurupu hayo yalikuwa yanalipwa na hospitali moja kwa moja kwao  kutoka katika malipo wanayolipa wagonjwa kutona kupatiwa ushauri au matibabu,” imesema taarifa hiyo.

Taarifa inasema kuwa mtu akipita katika mazingira ya hospitali ya Bikoro anaweza kuona wagonjwa wakiwa wamekaa katika viti kwa saa kadhaa bila kuhudumiwa ambapo wiki chache zilizopita, mgonjwa mmoja alisema kuwa alisubiri saa nzima kupata matibabu.

Kwa takribani miezi mitatu, jimbo la Equateur lilikumbwa na mlipuko wa Ebola ambao ulisababisha watu 54 kuugua ugonjwa huo, 33 kati yao wakipoteza maisha na 21 maisha yao yakinusuriwa na wataalamu wa afya.

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter