Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Canada kuipiga jeki UNFPA Iraq kwa miaka mingine minne

Wahudumu wa afya wakisaidiwa UNICEF wakiwa katika ziara ya mama aliyejifungua mwanae mchanga huko Iraq.
UNICEF/UN032140/Mackenzie
Wahudumu wa afya wakisaidiwa UNICEF wakiwa katika ziara ya mama aliyejifungua mwanae mchanga huko Iraq.

Canada kuipiga jeki UNFPA Iraq kwa miaka mingine minne

Wanawake

Serikali ya Canada leo imetangaza mchango mwingine wa miaka 4 wa dola za Canada milioni 5 kwa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu UNFPA,  ili kusaidia kuzijengea uwezo taasisi za serikali ya Iraq kwa ajili ya utekelezaji wa masuala ya jinsia na afya ya uzazi nchini kote.

Licha ya kumalizika kwa operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la ISIL, athari za miaka mitatu ya vita kwa wanawake na wasichana nchini Iraq bado ni kubwa sana limesema shirika hilo.

Fedha hizo zitaiwezesha UNFPA kubadili huduma zake za mpito kuwa na mipango ya maendeleo ya muda mrefu ambayo itaboresha usawa wa kijinsia , kuwawezesha wanawake na kuongeza fursa na matumizi ya huduma za afya ya uzazi.

Kwa mujibu wa mkuu wa ushirikiano wa ubalozi wa Canada nchini Iraq aliyekabidhi msaada huo , wakati Iraq na watu wake lazima waendelee kushughulikia mahitaji ya dharura ya kibinadamu, ni lazima pia msukumo uwekwe katika kutoa vipaumbele vya muda mrefu na ni muhimu kwa maamuzi ya serikali ya Iraq na mfumo mzima wa afya ukazingatia na kutilia maanani huduma za uzazi na mahitaji ya wanawake na wasichana.

Naye mwakilishi wa UNFPA nchini Iraq  Ramanathan Balakrishnan, amesema mchango huo wa Canada ni muhimu hasa katika kuwakomboa wanawake wa taifa hilo walio na matatizo mengi ya afya ya uzazi na changamoto za ukatili wa kijinsia, lakini pia zitasaidia harakati ya uwezeshaji wa wanawake na kuchagiza juhudi za usawa wa kijinsia na haki ya afya ya uzazi.