Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake Iraq wako hatarini , majumbani, shuleni na maeneo ya umma:UNICEF/UNFPA

IOM ikitoa msaada kwa wanawake wakimbizi wa ndani mjini Baghdad Iraq
Picha: IOM
IOM ikitoa msaada kwa wanawake wakimbizi wa ndani mjini Baghdad Iraq

Wanawake Iraq wako hatarini , majumbani, shuleni na maeneo ya umma:UNICEF/UNFPA

Wanawake

Nchini Iraq wanawake na wasichana kutoka kila aina ya maisha wanasalia katika hatari kubwa ya kufanyiwa ukatili iwe majumbani, shuleni na katika maeneo ya umma.

Kwa mujibu wa utafiti wa pamoja uliofanywa na serikali ya Iraq na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF , asilimia 37 ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 15 na 49 nchini humo wanafikiri kwamba ukatili dhidi ya wanawake unakubalika, wakati utafiti mpya wa shirika la Umoja wa Mataifa la idadi ya watu duniani UNFPA ukionyesha kwamba asilimia 63 ya matukio ya ukatili wa kijinsia Iraq yanatekelezwa na watu wa familia.

Siku 16 za uhamasishaji kwa lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake zikiendelea UNICEF na UNFPA wamethibitisha nia yao ya kukomesha aina zote za ukatili dhidi ya wanawake. Peter Hawkins mwakilishi wa UNICEF Iraq amesema “ Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana ni ukiukwaji wa haki za binadamu na una athari katika afya zao, maisha yao na mustakabali wao. Kamwe hauwezi kuhalalishwa katika jamii.”

Ameongeza kuwa wanawake na wasicha ni nusu ya watu wote nchini Iraq na wana haki ya kuishi bila woga na ukatili na wanastahili kuwa huru kufikia uopeo wa uwezo wao katika maisha.

Watoto wakiwa ndani ya darasa la shule ya hema ya UNICEF katika kambi ya Alhabanya,Anbar, Iraq.Watoto wahamiaji na wakimbizi hukosa elimu wanakokimbilia.
UNICEF/UN0161150/Anmar
Watoto wakiwa ndani ya darasa la shule ya hema ya UNICEF katika kambi ya Alhabanya,Anbar, Iraq.Watoto wahamiaji na wakimbizi hukosa elimu wanakokimbilia.

Naye mwakilishi wa UNFPA nchini humo Dr. Oluremi Sognuro, ameongeza kuwa “Kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na wasichana sio chaguo bali ni wajibu wa muda mrefu na ni lazima uwe sehemu ya jamii ya Iraq kupitia juhudi za pamoja zetu sote. Tunapaswa kufanya kila tuwezalo kuwasaidia wanawake na wasichana kuwa na maisha yenye utu na ustawi.”

Mashirika hayo yamesema hatari zaidi p[ia iko katika maeneo ya wakimbizi wa ndani ambako ukatili wa kingono, udhalilishwaji na ndoa za utotoni huchukua nafasi kubwa na nchini Iraq wasichana wadogo kuanzia umri wa miaka 12 huozwa.

Hivi sasa UNICEF na UNFPA wanatoa huduma maalumu ikiwemo ya kisaikolojia kwa ajili ya waathirika wa ukatili wa kingono Iraq na wanafanya kazi kuzuia ndoa za utotoni . UNFPA pia imezindua line maalumu ya dharura kwa manusura wa ukatili kwenye jimbo la Kurdistan. Kwa pamoja wameitaka serikali ya Iraq kutoa huduma inayoiendana na umri kwa waathirika wa ukatili wa kingono na kijinsia , pia wameitaka iwe na sheria ya kusisitiza ukomeshaji wa ndoa za utotoni.