Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNITAD yaendelea na maandalizi kabla ya kazi rasmi inayotarajiwa mwakani

Vita nchini Iraq na mashambulizi yaliyoongozwa na ISIL  yalisababisha watoto pia kupokwa  haki zao za msingi
UNICEF/UN0127481/Anmar
Vita nchini Iraq na mashambulizi yaliyoongozwa na ISIL yalisababisha watoto pia kupokwa haki zao za msingi

UNITAD yaendelea na maandalizi kabla ya kazi rasmi inayotarajiwa mwakani

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limepokea ripoti ya kwanza ya Jopo lililoundwa na baraza hilo kuchunguza na kuwajibisha uhalifu uliotekelezwa Iraq na kundi la ISIL au Daesh, UNITAD.

 Akiwasilisha ripoti hiyo Mshauri Maalum wa Katibu Mkuu na Mkuu wa jopo hilo Karim Asad Ahmad amesema kikubwa ambacho wamefanya ni maandalizi ya awali kabla ya kuanza rasmi kwa uchunguzi huo unaofuatia ombi la serikali ya Iraq.

Amesema maandalizi hayo ni pamoja na dira ambayo kwayo itahakikisha “mosi, tunakuwa na timu ambayo inafanya kazi yake kwa uhuru, bila upendeleo na inayowajibika kwa viwango vya juu vinavyowezekana, na pili kuhakikisha kuwa tunafanya kazi yetu kwa ushirikiano na uratibu wa serikali ya Iraq kwa kuheshimu mamlaka yake na kwa njia ambayo inatumia vyema vipaji na usaidizi kutoka pande zote za jamii ya Iraq.”

WATENDAJI WAWE WA KITAIFA NA KIMATAIFA

Ili kuhakikisha timu yao inakuwa jumuishi, Bwana Ahmad amesema, “mahitaji yamebainishwa juu ya watendaji wa kitaifa na kigeni na mchakato wa awali wa ajira unaendelea. Katika hili,, napenda kusisitiza kwa Baraza lizingatie kuwa ni muhimu kujumuisha kwenye timu hii, raia wa Iraq wenye ueledi.”

Bwana Ahmad amesema wakati wa zaira yake ya kwanza huko Iraq mwezi Agosti mwaka huu baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo alikutana na viongozi waandamizi wa serikali, manusura, vikundi vya kiraia, waumini wa Kikristu, madhehebu ya Shia, Suni, Turkmen, Kakai na jamii za kiyazidi ambazo amesema baada ya majadiliano alisisitiza kuwa sauti ya kila mwananchi itatumika kujenga ripoti ya maamuzi ya UNITAD.

Karim Asad Ahmad Khan, Mshauri Maalum na Mkuu wa jopo la uchunguzi la kuendeleza uwajibikaji wa uhalifu uliotekelezewa na ISIL nchini Iraq, akihubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
UN /Rick Bajornas
Karim Asad Ahmad Khan, Mshauri Maalum na Mkuu wa jopo la uchunguzi la kuendeleza uwajibikaji wa uhalifu uliotekelezewa na ISIL nchini Iraq, akihubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

VIPAUMBELE

Mkuu huyo wa UNITAD amesema sasa wanasubiri kwa hamu kuendelea na maandalizi tayari kwa uchunguzi unaotarajiwa kuanza mapema mwaka 2019 na kwamba vipaumbele vyao baada ya kukutana na viongozi wa serikali ya Iraq, na wadau wengine wakiwemo manusura wa  ukatili wa ISIL ni, “kukamilisha miundombinu ya kufanikisha utendaji ikiwemo ofisi za UNITAD na vifaa vinavyotakiwa, kukamilisha miundo muhimu ili uchunguzi uweze kuanza, kukusanya na kuchambua nyaraka za ushahidi wa vitendo vya  uhalifu kutoka vyanzo muhimu ikiwemo mamlaka za kitaifa, mashirika ya kimataifa na ya kiraia ili kubaini pengo lililopo.”

Ametumia hotuba yake kuhakikishia wajumbe ueledi ambao watazingatia katika kufanya kazi  yao akisisitiza kuwa, “hakuna mkinzano wowote katika kusimamia  uhuru huku wakiunga mkono harakati za uwajibikaji za kitaifa,” akisihi Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa liidhinishe bajeti yao ya dola milioni 21.5 milioni.

UNITAD

Tarehe 21 mwezi Septemba mwaka 2017, azimio namba 2379 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa  lilimtaka Katibu Mkuu wa UN kuanzisha jopo la uchunguzi la kusaidia mamlaka za Iraq kuwajibisha ISIL kwa uhalifu uliotendeka nchini humo kwa kukusanya na kuhifadhi ushahidi wa vitendo hivyo nchini Iraq, ushahidi ambao utathibitisha kuwa vitendo hivyo ni uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya halaiki.

Jopo hilo ndio UNITAD na lina jukumu la kusongesha uwajibika kimataifa kwa vitendo vyovyote vilivyofanywa na ISIL ili kukabiliana na dhana inayoenezwa na kundi hilo hadi kusababisha watu kujiunga nalo.