Hali nchini Yemen yazidi kudorora, Guterres apaza sauti

4 Disemba 2017

Nchini Yemen hali ya usalama na kibinadamu inazidi kuzorota kila uchao ambapo mapigano ya hivi karibuni yakiambatana na mashambulizi kutoka angani yamesababisha vifo vya raia na wengine wengi wamejeruhiwa.

Kufuatia kitendo hicho Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameeleza hofu yake kubwa kutokana na kuongezeka kwa mapigano huku yakizuia watu kutembea na misaada ya kibinadamu kufikia wahitaji.

Kupitia msemaji wake, Katibu Mkuu ameweka bayana kuwa hali hiyo inasababisha pia magari ya kubeba wagonjwa na wahudumu wa afya kushindwa kufikia majeruhi na raia hawawezi kutoka nje ili kujipatia mahitaji muhimu ikiwemo chakula.

Bwana Guterres ametoa wito kwa pande zote kinzani nchini Yemen kusitisha mashambulizi yote ya ardhini na angani kwa kuzingatia kuwa machungu waliyopata raia baada ya mipaka kufungwa tangu tarehe 6 mwezi uliopita na kufunguliwa kiasi hivi karibuni bado yapo.

Ametaka pande hizo kulinda raia kwa mujibu wa sheria za kibinadamu za kimataifa na kukumbusha kuwa hakuna suluhu ya kijeshi kwenye mzozo huo ambao ni mwaka wa tatu sasa tangu  uanze.

image
Huduma za kijamii ikiwemo maji safi na salama zimesalia za matatizo nchini Yemen huku watoto wakilazimika kutumia maji yasiyo safi wala salama. (Picha;Unicef-Yemen)

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter