Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Walinda amani watatu wa MINUSMA wauawa Mali na wengine kujeruhiwa

Maafisa wa UNPOL wa kikosi cha Senegal wanapiga doria nchini Mali. Picha MINUSMA / Marco Dormino

Walinda amani watatu wa MINUSMA wauawa Mali na wengine kujeruhiwa

Mapema leo asubuhi walinda amani watatu wa mpango wa Umoja wa Mataifa nchini Mali MINUSMA wameuawa nawengine wengi kujeruhiwa huku baadhi wakitajwa kuwa katika hali mahtuti baada ya kushambuliwa kwenye jimbo la Menaka umesema mpango huo.

Kwa mujibu wa MINUSMA shambulio hilo limetokea wakati MINUSMA na jeshi la serikali ya Mali FAMAS wakiwa katika operesheni ya pamoja ya ulinzi wa raia katika eneo hilo ambayo pia ilikuwa na lengo la kutoka huduma za afya zinazohitajika na wakazi wa jimbo la Menaka.

Washambuliaji kadhaa pia waliuawa wakati wakati walinda amani na jeshi la serikali ya Mali walipojaribu kujibu mashambulizi ambapo askari mmoja wa FAMAs naye alipoteza maisha.

Ndege za kijeshi za usaidizi zilipelekwa mara moja kwenye tukio kuimarisha usalama na kusafirisha majeruhi.

Mwakilishi maalumu wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa na mkuu wa MINUSMA Mahamat Saleh Annadif,amelaani vikali shambulio hilo na kutuma salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza Maisha huku akiwatakia ahuweni ya haraka majeruhi.