Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ongezeko la Idadi ya watoto Afrika laweza kuwa faida au janga- UNICEF

Ongezeko la Idadi ya watoto Afrika laweza kuwa faida au janga- UNICEF

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limesema makadirio mapya ya ongezeko kubwa la idadi ya watoto barani Afrika ifikapo mwaka 2030 yanaweza kuleta nuru au janga kulingana na hatua zitakazochukuliwa na serikali za bara hilo.

Ikipatiwa jina Kizazi 2030 Afrika-kupatia kipaumbele watoto ili kunufaika, ripoti hiyo inakadiria kuwa watoto barani Afrika ikiwa ni watu wote wenye umri wa chini ya miaka 18 wataongezeka na kufikia milioni 750 ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni nyongeza ya watoto milioni 170 ikilinganishwa na sasa.

Leila Pakkala ambaye ni Mkurugenzi wa UNICEF kanda ya Kusini na Mashariki mwa Afrika amesema kwa mantiki hiyo serikali zinatakiwa kuweka sera madhubuti za kuhakikisha idadai hiyo inaleta manufaa badala ya janga.

Ametaja uwekezaji katika mambo makuu matatu ambayo ni afya, elimu na ulinzi sambamba na uwezeshaji wa watoto wa Kike na wanawake.

Kwa mantiki hiyo Bi. Pakkala amesema Afrika inatakiwa kupatia mafunzo wahudumu wapya wa afya milioni 4.2 sambamba na walimu wapya milioni 5.3 katika miaka 13 ijayo ili kukidhi mahitaji yanayoibuka kutokana na ongezeko la watoto.

Mkurugenzi huyo wa kanda ya Afrika amesema kuwekeza katika afya, elimu na ulinzi wa mtoto lazima iwe kipaumbele cha Afrika kati ya sasa na mwaka 2030 la sivyo mustakhbali wa watoto na bara hilo utatumbukia.

Ripoti hiyo inasema kwa kufanya hivyo, pamoja na kuchagiza fursa za ajira kwa kuwekeza ndani na nje ya bara hilo, Afrika inaweza kushuhudia kuongezeka kwa pato la taifa mara nne ifikapo mwaka 2050.