Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

AMISOM yakusanya damu kusaidia wahanga wa shambulio Somalia

AMISOM yakusanya damu kusaidia wahanga wa shambulio Somalia

Kufuatia shambulio la kigaidi lililofanywa na Al Shabaab huko Mogadishu, Somalia Jumamosi na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 300 na wengine zaidi ya 500 kujeruhiwa, ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini humo, AMISOM umeendesha kampeni ya utoaji damu ili kusaidia majeruhi. Selina Jerobon na taarifa kamili.

(Taarifa ya Selina)

Nats..

Eneo liitwalo makutano ya kilometa Tano kwenye mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, sasa limegeuka magofu…mashambulizi ya Al-Shabaab yaliyosababisha vifo na majeruhi..

Kazi ya kuondoa vifusi ikiendelea…..ujumbe wa Muungano wa Afrika nchini Somalia, AMISOM nao umekusanya damu kutoka kwa maafisa wake na raia.

Damu hii ni kwa ajili ya mamia ya majeruhi waliolazwa kwenye hospitali tofauti mjini Mogadishu…

Mkuu wa masuala ya kitabibu wa AMISOM Dkt. Boniface Mandishona, amesema tayari wameweka mpango mahsusi wa usaidizi..

(Dkt. Boniface Mandishona)

 “Tunavyozungumza, tuko kwenye mchakato wa kukusanya damu kwenye makao makuu ya kikosi chetu kwa ajili ya wale waliojeruhiwa. Jana tulikuwa uwanja wa taifa tukikusanya damu. Tumeondoa askari kwenye hospitali yetu ili kupokea zaidi raia iwapo itahitajika.”

Wakati  huo huo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia umesema vijana nao wamejitokeza kusaidia kazi ya kuondoa vifusi kufuatia shambulio hilo kubwa zaidi kuwahi kukumba Somalia.