Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wachache Yemen wananufaika na vita ilhali wananchi wanafukarika- Ahmed

Wachache Yemen wananufaika na vita ilhali wananchi wanafukarika- Ahmed

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeombwa litumie shinikizo lake la kiuchumi na kisiasa dhidi ya pande kinzani nchini Yemen ili kumaliza machungu yanayokabili wananchi kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo.

Mjumbe maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismael Ould Cheikh Ahmed amewasilisha ombi hilo hii leo wakati akihutubia Baraza hilo jijini New York, Marekani.

Amesema ni dhahiri shairi kuwa kinachoendelea Yemen ni mwiba kwa raia wa kawaida na kwamba..

“Idadi kubwa ya wayemen wenye mamlaka wananufaika na mzozo huu ilhali raia wanakumbwa na machungu kuwahi kukumba Yemen. Wananchi wa Yemen wanataka vita hii ikome wakati ambao pengo kati yao na wale wenye madaraka au nguvu linazidi kupanuka. Vijana, wanawake na vikundi vya kiraia Yemen wanataka amani, utulivu na uwajibikaji kwa uhalifu uliotendeka.”

Hivyo amesema.. 

“Makubaliano ya kumaliza vita yanahitajika haraka ili serikali mpya ya umoja nchini Yemen inayoungwa mkono na jamii ya kimataifa iweze kuanza mchakato wa kujenga upya uchumi na taasisi za serikali.”

Hata hivyo mjumbe huyo maalum amepongeza hatua za hivi karibuni wakati wa kikao huko Ujerumani ambapo kulijadiliwa mbinu za kuinua uchumi wa Yemen kwa kuipatia tena uhai Benki Kuu ya nchi hiyo akisema itawezesha kulipa mishahara ya watumishi wa umma na hivyo kupunguza machungu ya kiuchumi na kibinadamu.