Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO yamteua Sumaya kuwa mjumbe wa sayansi kwa amani

UNESCO yamteua Sumaya kuwa mjumbe wa sayansi kwa amani

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu sayansi na utamaduni, UNESCO limemteua binti mfalme wa Jordan Sumaya Bint El Hassan kuwa mjumbe wake maalum wa sayansi kwa amani.

Hafla maalum ya kumtangaza imefanyika leo kwenye makao makuu ya UNESCO huko Paris Ufaransa ambapo atashika wadhifa huo kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2019.

Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Irina Bolova amesema uteuzi huo umefanyika baada ya shirika hilo kutambua mchango wa Sumaya wa kukuza sayansi na kutumia ushawishi katika kuhamasisha nchi kuchangia mabadiliko mazuri kwenye jamii na kuimarisha maendeleo ya kisayansi katika nchi yake ya asili.

Sumaya ambaye ni mhitimu wa taasisi ya sanaa ya Courtauld, amekuwa  Rais wa taasisi ya sayansi ya kifalme tangu mwaka 2006 na pia  mwenyekiti wa Baraza Kuu la Jordan la Sayansi na Teknolojia linaloshauri serikali kuhusu  masuala ya sera ya umma  katika sayansi na teknolojia.

Kama Mjumbe maalum wa UNESCO, Sumaya ataunga mkono kazi za shirika hilo katika ngazi ya diplomasia ya sayansi, hasa wakati wa mkutano wa sayansi wa dunia utakaofanyika mwezi ujao huko Jordan kuanzia tarehe 7  hadi 11.