Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF yahitaji dola milioni 76.1 Kusaidia watoto wa Rohingya

UNICEF yahitaji dola milioni 76.1 Kusaidia watoto wa Rohingya

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa ombi la zaidi ya dola milioni 76 ili kusaidia watoto walioathiriwa na janga linalokumba watu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar ambao sasa wanakimbilia kusini mwa Bangladesh.

Ufadhili huo utawezesha kukabiliana na mahitaji ya dharura kwa watoto 720,000 wa Rohingya wanaowasili ikiwemo wale waliowasili awali na watoto walio hatarini.

Kwa mujibu wa UNICEF asilimia 60 ya takriban wakimbizi laki tano wa Rohingywa waliokimbia Myanmar tangu Agosti 25 wanakadiriwa ni watoto. Wengi wao wanaishi katika mazingira duni na katika kambi za muda zilizotapakaa katika wilaya ya Cox Bazar.

Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF, Anthony Lake amesema watoto waliokata tamaa na familia zao wanakimbia  machafuko kila siku na UNICEF inajizatiti kukabiliana na mahitaji mengi lakini wanahitaji msaada ili kuweza kukidhi mahitaji kwa watoto hao ambao wanaporwa utoto wao.

Bwana Lake ambaye yuko ziarani nchini Bangladesh amesema wanahitaji msaada ili kusaidia watoto hao kuwa na mustakabali bora.