WHO na WFP wapo Bangladesh kutoa huduma kwa wakimbizi

26 Septemba 2017

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yameendelea kuongeza usaidizi wao kwa watu wa kabila la Rohingya ambao wamekimbilia Bangladesh kutokana na mateso wanayopata nchini mwao.

Mojawapo ya mashirika hayo ni lile la afya ulimwenguni WHO ambalo limesema limesaidia uanzishwaji wa chumba maalum cha  ufuatiliaji wa huduma za dharura  kwa wakimbizi kwenye wilaya ya Cox Bazar iliyopo Bangladesh.

Chumba hicho ambacho kinasaidia kudhibiti na kutambua kikamilifu hali ya afya ya wagonjwa , kutoa tahadhari mapema juu ya kuenea  na kuzuka kwa majanga na pia kuruhusu ufanisi na uratibu wa watendaji mbalimbali wa afya chini, kinatoa fursa kwa wahudumu kushirikiana na serikali ya Bangladesh katika kuendesha shughuli za afya kwa wakimbizi.

Katika jitihada hizo WHO itatoa vifaa muhimu vya matibabu na madawa kwa timu 20 kati ya 38 zinazohudumia makazi  ya wakimbizi kambini .

Ili kufanikisha shughuli zao WHO inatoa wito kwa wahisani kuchangia dola milioni 5.3 kwa miezi sita ijayo.

Nalo shirika la mpango wa chakula, WFP limetia nanga nchini Bangladesh kutoa msaada wa chakula kwa wakimbizi kwenye eneo hilo la Cox Bazar.

Mpaka sasa WFP imeandikisha watu 460,000 ambapo kila mmoja anapatiwa kilo 25 za mchele kila wiki mbili, kwa miezi sita ijayo.

Tayari kila mtu amepatiwa angalau mchele mara moja huku WFP ikisema inapatia kipaumbele  wanawake na watoto, halikadhalika familia zenye watoto wadogo, wajawazito na wanawake wanaonyonyesha.

Hata hivyo WFP imesema inahitaji dola milioni 72.7 ili kufadhili mahitaji ya watu zaidi ya milioni 1 kwa miezi sita  ijao.

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter