Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO yasaidia usafirishaji wa vifaa vya kuandikisha wapiga kura DRC

MONUSCO yasaidia usafirishaji wa vifaa vya kuandikisha wapiga kura DRC

Huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO umesaidia tume ya taifa ya uchaguzi kusafirisha vifaa vya kuandikisha wapiga kura hadi jimbo la Lomami.

Taarifa ya MONUSCO imesema operesheni hiyo imefanikishwa kwa usaidizi pia wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP ambapo helikopta ya MONUSCO imesafirisha tani zaidi ya 5,000 ya vifaa hivyo kuelekea Mbujimayi kwenye jimbo hilo.

Vifaa hivyo ni pamoja na makaratasi ya kuandikisha na vifaa vya ofisi.

Kuwasili kwa vifaa hivyo huko Wikong, eneo la Luilu jimbo la Lomami kutawezesha kuanza kwa mchakato wa kuandikisha wapiga kura jimboni humo.

Uchaguzi mkuu nchini DRC unatarajiwa kufanyika mwezi Aprili mwakani.