Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Swaziland kutokomeza Malaria ifikapo 2020

Swaziland kutokomeza Malaria ifikapo 2020

Swaziland imesema iko kwenye mwelekeo wa kutokomeza ugonjwa wa Malaria ifikapo mwaka 2020, ikiwa ni miongoni mwa nchi 8 kwenye ukanda wa Kusini mwa Afrika zilizo katika hatua za kuondokana na ugonjwa huo hatari.

Mfalme Mswati wa III amesema hayo hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York, Marekani wakati wa kikao cha ngazi ya juu kilichojadili dhima ya uongozi katika kutokomeza Malaria barani Afrika.

 (Sauti ya Mswati III)

“Sisi ni miongoni mwa nchi za mwanzo kabisa barani Afrika kuandaa kadi maalum ya kuonyesha mwelekeo wa kutokomeza Malaria. Na hii inarahisisha uwajibikaji na ufuatiliaji wa Malaria. Serikali imeendelea kutenga rasilimali za kitaifa kwa ajili ya kutekeleza mkakati wa kutokomeza Malaria.”

Mfalme Mswati ambaye pia ni mwenyekiti wa sasa wa Muungano wa viongozi wa Afrika dhidi ya Malaria, ALMA, amesema Swaziland imeweza kupata mafanikio hayo kutokana na usaidizi kutoka kwa wadau mbali mbali na hivyo…

(Sauti ya Mswati III)

“Tumeweza kutumia teknolojia bunifu katika kupanga upya mifumo yetu ya kubaini visa vyote vya malaria kwenye vituo vya afya na ngazi ya jamii ili kuhakikisha taarifa zinatolewa mapema na hatua ziweze kuchukuliwa.”

Mkutano huo umeandaliwa na muungano wa viongozi wa Afrika dhidi ya Malaria, ALMA kwa kushirikiana na wadau ikiwemo mpango wa kutokomeza Malaria Roll Back Malaria.

Swaziland ni miongoni mwa nchi 8 za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambazo zimejiwekea lengo la kutokomeza Malaria kupitia ushirikiano baina yao.  Nchi nyingine ni Botswana, Msumbiji, Namibia, Afrika Kusini, Swaziland, Zambia, na Zimbabwe.