Haki ipatikane kwa wahanga wa mauaji huko Kamanyola - Sidikou

18 Septemba 2017

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC MONUSCO umetaka uchunguzi ufanyike ili kubaini wahusika wa mauaji ya wasaka hifadhi 30 wa Burundi huko jimbo la Kivu Kusini. Joseph Msami na ripoti kamili.

(Taarifa ya Msami)

Maelfu ya wakimbizi wa Burundi walifika eneo la Kamanyola huko Walungu jimbo la Kivu Kusini kwa usalama wao.

Hata hivyo yaripotiwa kuwa wakiwa eneo hilo walifika katika ofisi ya usalama wa taifa ili kufahamu hatma ya wakimbizi wenzao walikuwa wanashikiliwa kwenye kituo hicho.

Habari zinasema punde baada ya kufika ofisi hiyo mzozo ulizuka baina yao na jeshi la serikali FARDC na polisi ambapo wasaka hifadhi 30 waliuawa na 26 walijeruhiwa.

Tayari mazishi yamefanyika huku MONUSCO ikisaidia matibabu na kusafirisha majeruhi waliokuwa katika hali mbaya hadi hospitali huko Bukavu.

Mkuu wa MONUSCO Maman Sambo Sidikou amesema ni lazima sheria ichukue mkondo wake na wahanga wa tukio hilo wapate haki.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter