Idadi ya waliouawa Iraq yapungua- UNAMI

Idadi ya waliouawa Iraq yapungua- UNAMI

Idadi ya raia waliouawa au kujeruhiwa nchini Iraq imeshuka kwa viwango vya chini kabisa , kwa mujibu wa takwimu zilizochapishwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Iraq (UNAMI)

Jumla ya raia 125 waliuawa mwezi Agosti huku wengine 188 walijeruhiwa kwa sababu ya visa vya ugaidi na mapigano kote nchini.

Hii inalinganishwa na vifo 241 vilivyoripotiwa mwezi Julai na vifo 415 mwezi Juni, licha ya kwamba sampuli ya takwimu sio thabiti kutoka mwezi mmoja hadi mwingine na UNAMI inasema haikuweza kupata takwimu za majeruhi wa mwezi Agosti kutoka mamlakaywa kiafya jimbo la Anbar

Mji mkuu Baghdad umetajwa kama jimbo lilokuwa na waathirika wengi idadi ikiwa ni 180 ikifuatiwa na Ninewa ambako watu 36 waliuawa na wengine 18 walijeruhiwa.

Operesheni za serikali ya Iraq dhidi ya miji inayodhibitiwa na magaidi wa Daesh zimekuwa zikiendelea kwa muda kufuatia ukombozi wa mji wa Mosul.

Kufuatia kulengwa kwa raia wasio na hatia mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu nchini Iraq Ján Kubiš amelaani  vitendo hivyo akisema kwamba magaidi wa Daesh wanalipiza kisasi cha kushindwa kwao kupitia raia.

Aidha ameongeza kwamba utulivu na uvumilivu wa watu wa Iraq umeshinda juhudi za magaidi kuvunja umoja wao.

Halikadhalika bwana Kubiš amepongeza watu na serikali ya Iraq kwa ukombozi wa mji wa Tal Afar kutoka kwa Daesh, au ISIL na kupongeza jeshi la Iraq kwa juhudi zao za kipekee katika kulinda Maisha ya raia.

Kubiš amesema kipaumbele katika maeneo yaliyokombolewa ni kuhakikisha raia wanarudi nyumbani na kuanza mchakato wa kujenga upya maisha yao.