Msaada wa dharura sio muoarubaini wa janga la njaa Ethiopia-FAO

Msaada wa dharura sio muoarubaini wa janga la njaa Ethiopia-FAO

Takriban watu milioni 8.5 nchini Ethiopia wanahitaji msaada wa chakula katika nusu ya mwaka huu wa 2017 lakini uhaba wa chakula unaoshuhudiwa hauwezi kutatuliwa na msaada wa dharura pekee. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Hii ni kwa mujibu wa shirika la chakula duniani FAO likiongeza kuwa suluhu ya kudumu ni kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na  hatari na kuzuia kutumbukia katika janga.

Ripoti hii inakuja wakati ambapo wakuu wa mashirika ya Umoja wa lile la chakula na kilimo, FAO, maendeleo ya kilimo IFAD na mpango wa chakula, WFP wakizuru Ethiopia.

José Graziano da Silva wa FAO, Gilbert F. Houngbo wa IFAD na David Beasley wa WFP wanatathmini hali ya janga na kujadili mbinu za kuwezesha serikali ili iweze kukabiliana na mahitaji ya kibinadamu na kupunguza madhara ya majanga katika siku za usoni.

Mmoja wa waathirika ni Mohammed ambaye ni mfugaji na amesema kuwa ukame unaoikumba Ethiopia umeathiri maisha yao na anachojitaji yeye ni kuokoa mifugo yake ili akidhi maisha.

Mohammed ni mkazi wa kijiji cha Dolobata eneo la Somali nchini Ethiopia ambako mvua hazijanyesha kwa mwaka wa tatu mfululizo na viwango vya njaa na utapiamlo vinapanda kwa kasi kubwa.

FAO imesaidia watu nusu milioni kwa njia kadhaa ikiwemo kuwapatia chakula cha mifugo na tiba za kuzuia magonjwa.