Bangladesh fungulieni mipaka warohingya wanaokimbia ghasia Myanmar

29 Agosti 2017

Umoja wa Mataifa umesema bado kuna tatizo kubwa kuwafikia waliokumbwa na ghasia kwenye jimbo la Rakhine nchini Myanmar wakati huu ambapo hali ya usalama inazidi kuzorota kutokana mapigano kati ya waumini wa kibuda walio wengi na waislamu ambao ni wachache.

Ghasia ziliibuka kwenye eneo la kaskazini-magharibi mwa jimbo hilo siku ya ijumaa baada ya majengo ya polisi kushambuliwa ambapo watu kadhaa walifariki dunia wakiwemo maafisa wa ulinzi na usalama.

Kufuatia hali hiyo kamishna mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein ameeleza wasiwasi wake kuhusu hali hiyo akitaka viongozi wa kisiasa nchini humo washutumu vitendo hivyo pamoja na uchochezi unaoendeshwa kupitia mitandao ya kijamii.

Nalo shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR limesema ghasia za hivi karibuni zimesababisha watu zaidi ya 5,000 kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh na maelfu kadhaa wako mpakani.

Msemaji wa UNHCR Geneva, Uswisi, Adrian Edwards anasema kuna ripoti baadhi ya wananchi wanazuiwa kuingia Bangladesh.

(Sauti ya Adrian)

“Hii ni hatari sana kwa waathirika. Bangladesh kwa miongo kadhaa imehifadhi wakimbizi kutoka Myanmar. UNHCR inaamini kuwa ni muhimu sana kuendelea kuruhusu warohingya wanaokimbia ghasia kusaka hifadhi nchini humo.”

 

♦ Kutembelea ukurasa maalum wa UNGA76 bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter