Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mazungumzo na Kiir yamekuwa mazuri lakini bado tunawasiwasi: Lacroix

Mazungumzo na Kiir yamekuwa mazuri lakini bado tunawasiwasi: Lacroix

Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani za Umoja wa Mataifa, Jeane-Pierre Lacroix, amesisitiza haja ya ushirikiano wa serikali ya Sudan Kusini katika kuhakikisha uhasama nchini humo unafikia ukomo.

Akizungumza na waandishi wa habari,baada ya kukutana leo hii na rais Salva Kiir katika makao makuu ya jeshi la SPLA huko Bilpha Lacroix amesema baadhi ya mambo waliyojadili ni kuhusu hali ya usalama akisema ameridhishwa na hatimaye kupelekwa kwa jeshi la ulinzi wa taifa RPF, hali ya kibinadamu nchini humo, mchango wa Uganda wa kuunganisha tena majeshi ya SPLA pamoja na umuhimu wa kuimarisha makubaliano ya amani.

Amesema mazungumzo na rais yamekuwa mazuri na yenye matumaini lakini kuna maeneo ambayo bado Umoja wa Mataifa haujaridhika nayo..

(Cut ya Lacroix)

"Kuhusu usalama, bila shaka, tunawasiwasi kuwa makubaliano ya usitishaji mapigano hayatekelezwi katika maeneo yote, na rais ametueleza maoni yake na tunatumai kuwa usalama utarejea katika maeneo yaliyoathirika, na kuhusu hali ya kibinadamu, ni hali ambayo bado umoja wa mataifa unawasiwasi mkubwa , na Umoja wa Mataifa unajitahidi kutoa msaada kadri ya uwezo wake bila ya kubagua".

Bwana Lacroix ameupongeza Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNMISS kwa kazi nzuri, wadau wa masuala ya kibindamu na mashirika ya Umoja wa Mataifa na anatarajia ushirikiano mzuri na serikali ya Sudan Kusini akisema kuwa hii ni nchi yao na Umoja wa Mataifa upo hapo tu kuwasaidia kupata amani.