Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Juhudi za pamoja zinahitajika kutatua mzozo wa kisiasa Burundi-Kafando

Juhudi za pamoja zinahitajika kutatua mzozo wa kisiasa Burundi-Kafando

Juhudi zote ambazo zinaelekezwa kwa ajili ya kutatua mzozo wa kisiasa nchini Burundi lazima zishirikishe viongozi barani Afrika na hususan walioko katika ukanda huo.

Hiyo ni kwa mujibu wa Mjumbe maalumu wa katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa nchini Burundi Michel Kafando akihutubia kikao cha Baraza la Usalama kuhusu hali nchini Burundi. Bwana Kafando amesema amepata fursa ya kutembelea Burundi ambako amekutana na viongozi wa serikalini ikiwemo rais Pierre Nkurunziza, upinzani na vyama vya kiraia na kusema licha ya kwamba hali ya utulivu imerejea katika mji mkuu Bujumbura lakini mashambulizi ya vilipuzi hivi majuzi yanatia hofu.

Akihutubia Baraza hilo kwa mara ya kwanza katika wadhfa huo, mjumbe huyo amesema baada ya kuzungumza na mamlaka Burundi, na wapatanishi wa mzozo wa nchi hiyo, Rais wa Uganda Yoweri Museveni na Rais Mstaafu wa Tanzania Benjamin Mkapa, kupitia mkalimani amesema ili kuwe na hali ya utulivu Burundi kile kinachohitajika kutatua mzozo wa kisiasa ni…

(Sauti ya Kafando)

“Kwanza ni kuhakikisha mazungumzo jumuishi, ni muhimu kwamba serikali ya Burundi isikilize wito wa nchi kwenye ukanda huo na muungano wa Afrika kwa msaada wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha mazungumzo jumuishi na hiyo inamaanisha kushirikisha vyama vya upinzani vilivyoko nje na ndani ya nchi, kwa mtazamo wangu hii ndio gharama tunayohitaji kulipa ili kujenga upya imani ya watu wa Burundi kwa ajili ya taasisi thabiti na zinazozingatia demokrasia na kuwezesha maridhiano ya kitaifa.”

Hali kadhalika bwana Kafando amesisitiza kuwa suluhu ya kudumu ya mzozo wa kisiasa nchini humo ni lazima izingatie misingi ya makubaliano ya Arusha kuhusu Burundi yanayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa na ukanda wa maziwa makuu.