Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mgogoro wa kibinadamu DRC wafurutu ada:O’Brien

Mgogoro wa kibinadamu DRC wafurutu ada:O’Brien

Kumekuwa na ongezeko kubwa la mgogoro wa kibinadamu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, kwa mujibu wa mtaratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu Stephen O'Brien.

Ameyasema hayo wakati akihitimisha ziara yake ya siku nnne nchini DRC na kutoa wito kwa dunia kutoisahau nchi hiyo ambayo sasa ina idadi kubwa kabisa ya watu waliotawanywa na machafuko kuliko nchi nyingine yoyote barani Afrika.

Akiwa nchini humo Bwana O'Brien alitembelea baadhi ya jamii zilizoathirika na machafuko zikiwemo za Tshikapa kwenye jimbo la Kasai ambako mwaka mmoja wa vita na ukiukaji wa haki za binadamu umetawanya watu takribani milioni 1.4.

Ghasia katika majimbo matano yanayounda Kasai zimefanya maelfu ya watoto kuacha shule na kuripotiwa kwa visa 600 vya ukatili wa kingono tangu mwaka jana.

O’Brien amesema mamilioni ya wanaume , wanawake, wavulana na wasichana wameathirika kutokana na machafuko hayo kwa, magonjwa na utapia mlo.

(O’BRIEN CUT)

"Katika miezi 12 iliyopita tumeshuhudia kuongezeka kwa mgogoro huu mkubwa hapa DRC, kwa kweli idadi ya wakimbizi wa ndani imeongezeka kutoka milioni 2.2 na kufikia milioni 3.8 katika kipindi cha miezi sita tu, na sasa hii inawakilisha , idadi ya juu kabisa ya wakimbizi wa ndani kuliko nchi yoyote Afrika.”

Bwana O'Brien ametoa wito wa fursa salama kwa wahudumu wa misaada jasiri ambao wanafanya kila wawezalo kuhakikisha kwamba msaada unawafikia wanaouhitaji zaidi vijijini.

Mbali ya idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani , DRC pia inakabiliana na wimbi la wakimbizi kutoka nchi jirani za Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR na Sudan Kusini.