Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita, mateso, ghasia vyazidi kufurusha watu makwao- UNHCR

Vita, mateso, ghasia vyazidi kufurusha watu makwao- UNHCR

Idadi ya wakimbizi duniani imeongezeka mwaka 2016 na kufikia milioni 65.6, vichocheo vikitajwa kuwa ni vita, ghasia na mateso. Flora Nducha na ripoti kamili.

(Taarifa ya Flora)

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa ripoti ya mwelekeo wa wakimbizi duniani kwa mwaka 2016, ripoti iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR.

Takwimu zinaonyesha ongezeko kutoka milioni 65.3 mwaka 2015 ambapo Kamishna Mkuu wa UNHCR Filipo Grandi amesema mzozo wa Sudan Kusini umechochea ongezeko hilo, licha ya kwamba mzozo wa Syria ndio umesalia janga kubwa la ukimbizi.

Amesema idadi hiyo ya ongezeko la wakimbizi 300,000 inaonekana ni ndogo lakini kwa UNHCR..

(Sauti ya Grandi)

“Kutokupungua kwa idadi au ongezeko dogo ni habari mbaya kwa sababu inamaanisha kimsingi sababu za watu wengi kulazimishwa kukimbia makwao bado hazijaweza kushughulikiwa kwa ufanisi.”

UNHCR inasema katika kila sekunde tatu mtu mmoja anakuwa mkimbizi, iwe wa ndani, nchi jirani au msaka hifadhi.