Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wataalamu wa ICT wabonga bongo kuhusu SDGs

Wataalamu wa ICT wabonga bongo kuhusu SDGs

Zaidi ya wataalamu 2,500 wa teknolojia ya habari na mawasiliano ICT wanakutana mjini Geneva, Uswisi, kwa siku tano kuanzia jumatatu juma hili, ambapo wanabadilishana ujuzi na uzoefu lengo likiwa kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu SDGs.

Mkutano huo wa kimataifa kuhusu upashanaji wa taarifa (WSIS Forum 2017 ) , kwa mwaka huu ukiwa chini ya uenyekiti wa Rwanda, utaangazia zaidi namna ICT inavyoweza kutumiwa kutekeleza SDGs hususani katik elimu, uwezeshaji wa kijinsia, mazingira, miundombinu na ugunduzi.

Akizungumza katika mkutano huo Katibu Mkuu wa shirika la mawasiliano duniani ITU, Houlin Zhao, amesema majadiliano yanatarajiwa kuibua jitihada za nguvu ya ICT katika utekelezaji wa SDGs.

Mkutano huo pia utashuhudia kutangazwa kwa washindi wa tuzo ya WSIS kwa mwaka 2017, tuzo ambayo inatambua mafanikio endelevu na ambayo huandaliwa na ITU, shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni UNESCO, Kamati ya Umoja wa Mataifa ya bishara na maendeleo UNCTAD, mpango wa maendeleo wa Umoja wa Mataifa UNDP pamoja na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa.