Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Guterres asema utofauti ni mali na sio tishio

Guterres asema utofauti ni mali na sio tishio

Jamii zinazidi kutofautiana zaidi na zaidi ulimwenguni kote na hili ni lazima lizingatiwe kama kitu chanya,  amesema leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres wakati wa  ziara yake Kyrgyzstan.

Guterres alitembelea  eneo la Osh na kuweka shada la maua katika sanamu ijulikanayao kama “Machozi ya Mama”, iliyo kumbukumbu ya  mamia ya watu waliopoteza maisha yao wakati wa ghasia za kikabila baina ya Wakirgyzstan na Wauzbeskistan Juni 2010.

Akiwa Kamishna Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi, UNHCR alitembelea eneo hilo ambapo maelfu ya watu walilazimishwa kukimbia makwao kutokana na vita hivyo vya miaka saba.

Amesema jamii ya Osh wameonyesha ustahamilivu wa ajabu, uvumilivu mkubwa na uwezo mkubwa wa kujiponya mfano ambao ni lazima kuigwa.

Hata hivyo amesema ili utofauti huo ustawi ni lazima kuwekeza katika sekta za kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kidini, na katika  mwezi huu mtukufu wa Ramadhan, amekumbusha watu kila mahali kwamba amani na uvumilivu ni lazima utawale, kwani ndio taswira ya Uislamu.

Guterres amekutana na Rais wa Kyrgyzstan pamoja na kuhutubia jukwaa la mradi unaoutumia teknolojia ya hali ya juu katika huduma za umma unaojulikana kama Taza koom.

Jumamosi  Guterres alitembelea bahari ya Aral nchini Uzbekistan ambayo maji yake yamepungua kwa robo ya asili yake kutokana na matumizi mabaya ya kibinadamu, akishtushwa na janga hilo la kiikologia, na kusema iwe fundisho kwa ulimwengu wote na hamazisho kwa jamii za kimataifa kutekeleza mkataba wa Paris kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Kyrgyzstan ni sehemu ya mwisho ya ziara yake ya siku sita Asia ya Kati iliyoanza alhamisi iliyopita.