Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maisha ya watoto 40,000 shakani Ar Raqqa, Syria-UNICEF

Maisha ya watoto 40,000 shakani Ar Raqqa, Syria-UNICEF

Mashambulizi mazito mjini Ar-Raqqa nchini Syria yanatishia maisha ya zaidi ya watoto 40,000 ambao wanasalia mtegoni mwa hatari kubwa, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF.

UNICEF imesema imepokea taarifa za kutisha kwamba takribani watoto 25 wameuawa na kujeruhiwa katika mshambulizi ya hivi karibuni zaidi mjini humo, shule na hospitali zikiwa zimeshambuliwa, huku pia kukiwa na taarifa kwamba wanaojaribu kukimbia wako hatarini kuuawa au kujeruhiwa.

Msemaji wa shirika hilo mjini Genevea Uswisi Christopher Boulierac amewaambia waandishi wa habari kwamba vitendo huvyo dhalimu kwa watoto vina matokeo hasi ambapo   watoto wanapokwa haki zao za msingi za uokozi wa maisha, na msaada kidogo umewasili Ar-Raqqa tangu mwaka 2013 kutokana na ghasia na vikwazo dhidi ya misaada hiyo.’’

Machafuko mjini humo yamesababisha idadi kubwa ya waliofurushwa ambapo watoto karibu 80,000 hivi sasa ni wakimbizi wa ndani na wanaishi katika malazi na makambi ya muda.

UNICEF imezitolea wito pande kinzani katika mgogoro wa Syria kulinda watoto mjini Ar-Raqqa na kuwaruhusu wanaotaka kuondoka wafanye hivyo kwa usalama.