Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu milioni watia saini kupinga matumizi ya plastiki-UM

Watu milioni watia saini kupinga matumizi ya plastiki-UM

Kampeni ya Avaaz imetoa wito kwa serikali za dunia kupiga marufuku matumizi ya plastiki katika miaka mitano ijayo.

Kampeni hiyo ambayo imetiwa saini na watu milioni moja itawasilishwa kwa shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP ili kuunga mkono harakati zake za kuwa na bahari safi kwa kukomesha uchafu baharini.

Mkurugenzi wa UNEP Erik Solheim, atawasilisha hoja hiyo ya umma katika hotuba yake kwenye mkutano wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya bahari unaoendelea kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa hadi Juni 9 na pia atakapozungumza na serikali.

Hadi sasa nchi zaidi ya 20 zimejitokeza kuunga mkono kampeni hiyo #cleanseas inayozihimiza serikali, viwanda na raia kuacha matumizi ya kupindukia ya plastiki na kukomesha chembechembe za plastiki katika vipodozi ifikapo 2020 ambavyo vyote ni chanzo kikubwa cha uchafu baharini.

Bwana Solheim amesema ingawa nchi zaidi ya 20 zinaunga mkono kampeni hiyo bado nchi zaidi zahitajika endapo tutahitaji kupunguza kwa kiasi kikubwa tani milioni 8 za plastiki zinazoishia baharini kila mwaka na kusababisha tafrani inayohatarisha maisha ya viumbe wa majini.

Akiwashukuru waliotia saini kampeni hiyo Solheim ameaihidi kuhakikisha nchi zinaelewa watu duniani kote wanataka kupindua ukurasa kuhusu taka baharini.