Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanasiasa wasio na aibu wanasigina katiba za nchi zao - Zeid

Wanasiasa wasio na aibu wanasigina katiba za nchi zao - Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa Zeid Raa’d Al Hussein ameeleza masikitiko yake juu ya vitendo vya baadhi ya wanasiasa kutokuwa na aibu kutokana na matendo yao yanayoleta machungu kwa wananchi wao. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Masikitiko hayo ya Zeid yamo kwenye hotuba yake ya kurasa nane wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 35 wa Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa.

Hotuba ilisheheni mambo kadhaa ikiwemo hofu yake juu ya wataalamu wa haki za binadamu kukumbwa na vitisho au kuzuiwa kufanya kazi zao huko Iran, Myanmar na Ufilipino akisema hilo halikubaliki.

Ameangazia pia wanasiasa ambao amesema hawana aibu kabisa na vitendo vyao vya kupindisha sheria na kuacha wananchi wao wakiteseka kwa machungu kama vile ubakaji na kuuawa.

“Pindi viongozi wafananao na wezi wanapoingia madarakani iwe kidemokrasia au kwa njia nyingine na kupinga waziwazi siyo tu sheria zao na katiba, bali pia wajibu wao chini ya sheria za kimataifa…iko wapi aibu yao?”

Amekumbusha serikali kuwa kusimamia haki ni zaidi ya kutia saini mikataba ya kimataifa.