Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri na si porojo- Guterres

Mabadiliko ya tabianchi ni dhahiri na si porojo- Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema mabadiliko ya tabianchi ni wimbi kubwa linalokumba dunia hivi sasa na ni lazima lishughulikiwe ili kurejesha imani na usalama ulimwenguni.

Akifungua jukwaa la kimataifa la kiuchumi huko St. Petersburg nchini Urusi amesema ingawa baadhi ya nchi zinaamini kuwa mabadiliko ya tabianchi ni porojo zisizo na msingi wowote, ni lazima kuendeleza mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi licha ya shuku na shaka ya nchi hizo.

(Sauti ya Guterres)

"Tunaona mielekeo mikubwa sasa duniani- ongezeko la idadi ya watu, kasi kubwa ya kukua kwa miji, ukosefu wa uhakika wa chakula, uhaba wa maji, lakini zaidi ya yote ni mabadiliko ya tabianchi ambayo ndiyo yanachochea mielekeo yote hiyo mikubwa duniani.”

Bwana Guterres anasema sasa hata imani inatoweka hasa pale si kila mtu anatambua kuwa jamii ya kimataifa hivi sasa inapaswa kupatia kipaumbele cha juu mabadiliko ya tabianchi.

Amesema katika kuchagiza uchumi unaojali mazingira na sekta ya teknolojia ya viwanda inayokuwa, Urusi inaweza kuwa na dhima muhimu kama kitovu cha sayansi na teknolojia kwa zama zilizopita na sasa.