Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utipwatipwa unazidi kuongezeka katika vijana Ulaya – Ropiti ya WHO

Utipwatipwa unazidi kuongezeka katika vijana Ulaya – Ropiti ya WHO

Ripoti mpya ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) iliyozinduliwa leo kuhusu utipwatipwa nchini Ureno, imeonyesha kuwa idadi ya barubaru wenye utipwatipwa inazidi kuongezeka katika nchi nyingi katika ukanda wa WHO Ulaya.

Mkurugenzi wa WHO ukanda wa Ulaya, Dk. Zsuzsanna Jakab, amesema licha ya juhudi za kina za kupambana na utipwatipwa miongoni mwa watoto, mmoja kati ya kila barubaru watatu anakadiriwa kuwa na utipwatipwa barani Ulaya, viwango vikiwa juu zaidi kusini mwa Ulaya na nchi za eneo la Mediterania.

Amesema kinachotia wasiwasi hasa ni kwamba janga hilo linazidi kuongezeka katika nchi za mashariki mwa Ulaya, ambako viwango vilikuwa chini kwa miaka mingi.

Afisa huyo mwandamizi wa WHO amesema hatua kabambe za kisera zinapaswa kuchukuliwa ili kutimiza lengo la maendeleo endelevu la kusitisha ongezeko la utipwatipwa miongoni mwa watoto.

Utipwatipwa wa utotoni unachukuliwa kama mojawapo ya changamoto kubwa zaidi za afya ya umma ulimwenguni katika karne ya 21.