Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IOM yawatetea wahamiaji kwenye siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi dhidi ya LGBT

IOM yawatetea wahamiaji kwenye siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi dhidi ya LGBT

Kila mtu anapitia uhamiaji kwa namna tofauti, lakini jinsia na mtazamo wa kimapenzi vinaweza kuwa na athari kubwa katika safari ya mhamiaji, na kwa bahati mbaya athari hua ni mbaya na hata za hatari.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji, IOM, katika ujumbe maalumu wa siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi na chuki dhidi ya watu wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, waliobadili jinsia na wanaoshiriki mapenzi ya jinsia zote au LGBTI.

William Lacy Swing amesema mwaka 2017, watu wa LGBTI wameendelea kukabiliwa na ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwemo kutengwa, ubaguzi manyanyaso, udhalilishwaji hadharani, vifungo, ubakaji, kukosa huduma za afya, mateso, na mauaji.

Ameongeza kuwa nchi 75 bado zina sheria zinazoharamisha mapenzi ya jinsia moja na kutoa adhabu kali kwa watu hao ikiwemo kifo, na hizo zinaweza kuwa sababu za kwa nini watu wanahama au kutawanywa.

Bwana Swing amesema siku ya leo ni kumbusho kwamba usawa na uhuru dhidi ya ubaguzi ni haki za msingi za binadamu kwa wote bila kujali mtazamo wao wa kimapenzi au kama wamebadili jinsia.

Pia siku hii inakumbusha jinsi watu wa LGBTI wanavyokabiliwa na ghasia na ubaguzi kote duniani na kusisitiza kuchukua hatua za kuilinda jamii ya LGBTI.