Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi zaidi ya 20,000 wa DRC sasa wawasili Angola

Wakimbizi zaidi ya 20,000 wa DRC sasa wawasili Angola

Takriban wakimbizi 20,563 sasa wamewasili Angola, wakikimbia machafuko kwenye jimbo la Kasai nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, tangu mwezi Aprili.

Kwa mujibu wa shirika la kuhudumia wakimbizi UNHCR bado wakimbizi wanaendelea kuingia Angola wakivuka mpaka na kuingia Lundo jimbo la Luanda.

Jeshi la Angola limekuwa likiwasafirisha wakimbizi hao kutoka mpakani hadi kwenye vituo viwili vya mapokezi vya Cacanda na Moussunge. Andrej Mahecic ni msemaji wa UNHCR.

(SAUTI YA MAHECIC)

“Watu wanaowasili hivi karibuni ni pamoja na walio na vidonda vikubwa na majeraha ya kuungua, ambao wamepelekwa kwenye hospitali za karibu kupata huduma za haraka.Tayari hospitali hizo zimetibu watu 70 wenye vidonda na majeraha ya kuungua.”

UNHCR inaisaidia serikali ya Angola kubaini maeneo muafaka ya kuhamishia wakimbizi hao kutoka makazi ya muda, na imetoa ombi la dola milioni 6.5 ili kutoa huduma za kuokoa maisha ikiwemo chakula , lishe, afya na vifaa muhimu kwa wakimbizi