Skip to main content

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ziarani Uzbekistan

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ziarani Uzbekistan

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu katika Umoja wa Mataifa, Zeid Ra’ad Al Hussein, yupo ziarani nchini Uzbekistan, ikiwa ziara ya kwanza kabisa kufanywa na Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, tangu ofisi yake ilipoasisiwa mnamo mwaka 1993, miaka miwili baada ya Uzbekistan kujipatia uhuru, na mwaka mmoja baada ya nchi hiyo kujiunga na Umoja wa Mataifa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Bwana Zeid amesema ziara yake imekuwa fupi, lakini ilijumuisha mikutano mingi, ukiwemo mkutano muhimu wa kipindi cha saa moja na nusu na Rais Shavkat Mirziyoyev wa Uzbekistan. Amesema katika mkutano huo, walikubaliana kuhusu mambo kadhaa, zikiwemo hatua madhubuti za kuendeleza haki za binadamu nchini humo.

Moja ya makubaliano hayo ni kwamba sasa ofisi ya kikanda ya haki za binadamu sasa itashughulikia masuala ya nchi tano zilizopo kati mwa Bara Asia, badala ya nne tu ilivyokuwa imekubaliwa awali ilipofunguliwa ofisi hiyo mjini Bishkek mnamo mwaka 2008.

Zeid amesema kumekuwa na maendeleo taratibu katika uwanja wa haki za binadamu nchini Uzbekistan katika miaka minne iliyopita, licha ya changamoto kadhaa, akitaja sheria nyingi zilizopitishwa katika miezi minane iliyopita, na mkakati wa rais wa kuchukua hatua.

Mkakati huo wa rais unalenga kuboresha mfumo wa utawala wa umma, kuhakikisha utawala wa sheria na kurekebisha mfumo wa sheria, maendeleo na uhuru wa uchumi, kuendeleza sekta ya kijamii, pamoja na kuendeleza usalama, kuvumiliana kidini na kikabila, na sera nzuri katika masuala ya nje.