Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunawajibu wa kuwalinda raia wa Sudan Kusini: Meja Jenerali Mawut

Tunawajibu wa kuwalinda raia wa Sudan Kusini: Meja Jenerali Mawut

Serikali ya Sudan Kusini imemteua James Ajongo Mawut kuwa Meja Jenerali na mnadhimu mkuu wa jeshi la nchi hiyo, ambapo ametoa wito wa utulivu na kuwaahidi raia wa nchi hiyo kuwa atatumia fursa hiyo kurejesha amani nchini humo.

Akizungumza na radio Miraya ya Umoja wa Mataifa nchini humo, Meja Jenerali Mawut amesema anafahamu uzito wa jukumu hilo wakati huu ambapo nchi hiyo inakumbwa na vita na kwamba kuna vikwazo vingi lakini ....

(Sauti ya Meja Jenerali Mawut)

"Kwa kutumia vyema rasilimali nzuri ya binadamu tuliyonayo , kwa kuamini kuwa ni wazuri wakiwekwa mahala pazuri nina uhakika tutatoka katika janga hili. Sisi tuna jukumu la kikatiba kama jeshi la nchi hii kulinda raia na mipaka ya nchi"

Kuhusu suala la vikundi vyenye silaha, amesema atalishughulikia hilo kwa kuendana na yale yaliyokubaliwa katika mkataba wa amani, lakini kikwazo kilichopo ni fedha, akitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa na nchi jirani kusaidia serikali ya Sudan Kusini kifedha.