Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP yatoa neti za mbu milioni 6.5 Chad

UNDP yatoa neti za mbu milioni 6.5 Chad

Katika kuadhimisha Siku ya Malaria Duniani Jumanne April 25, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo , UNDP limetoa msaada wa vyandarua vya mbu vyenye dawa kwa raia milioni 13 nchini Chad kabla ya msimu wa mvua, eneo ambalo ungonjwa wa Malaria unaoongoza katika kusababisha vifo.

Kampeni hiyo kabambe ni sehemu ya maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu ambayo ni 'zuia malaria, okoa maisha', ambapo Shirika la Afya Duniani, WHO limesema takwimu zinaonyesha mbinu za kuzuia Malaria zimepunguza kasi ya ugonjwa huo, na hivyo limetoa wito wa kuziba pengo kwa kuongeza uwezo wa kuzuia kwa wale walio katika mazingira magumu.

Carol Flore Smerezniak ambaye ni Mkurugenzi wa UNDP Chad amesema ongezeko la mgogoro katika eneo la Ziwa Chad umesababisha ukosefu wa zana za kuzuia malaria kwa mamilioni ya watu.

(Sauti ya Carol)

"Kama mnavyojua kusini mwa jangwa la Sahara ndiko kumebebeba asilimia 90% ya ugonjwa wa malaria, na hususan Chad ndiyo iliyoathirika zaidi, na asilimia 97 ya watu wamo hatarini, na waliohatarini zaidi ni watoto chini ya umri wa miaka mitano, na wanawake wajawazito".