Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde kuondoka kwa UNAMID kusipoteze mafanikio- Mamabolo

Chonde chonde kuondoka kwa UNAMID kusipoteze mafanikio- Mamabolo

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limeelezwa kuwa mipango yoyote ya kuondoa ujumbe wa pamoja wa umoja huo na Muungano wa Afrika, AU huko Darfur, UNAMID uhakikishe hautatowesha mafanikio ya amani na utulivu yaliyokwishapatikana.

Mwakilishi wa pamoja wa Umoja wa Mataifa na AU huko Darfur, Jeremiah Mamabolo amesema hayo leo wakati akihutubia baraza hilo, ikiwa ni mara yake ya kwanza tangu ateuliwe kushika wadhifa huo.

Amesema ingawa Darfur ya leo ni tofauti na ile ya mwaka 2003 mapigano yalipoanza, bado kuna mapigano ya kikabila hapa na pale akitaja mizozo ya ardhi na rasilimali wakati wa msimu wa kilimo na kuhamahama kwa wafugaji.

Bwana Mamabolo amesema anafahamu kuwa Umoja wa Mataifa na AU wamepokea tathmini ya mapendekezo ya jinsi UNAMID itaondoka Darfur.

(Sauti ya Mamabolo)

“Hata hivyo, niruhusu mheshimiwa Rais, bila kuingilia matokeo ya tathmini ya mkakati huo, niseme kuwa kwa kuzingatia mazingira ya sasa Darfur, itakuwa vyema Umoja wa Mataifa na AU iangalie mkakati bora na unaotekelezeka wa kupanga upya UNAMID bila kupoteza mafanikio ambayo yameshapatikana hadi sasa.”

Bwana Mamabolo ambaye pia ni mkuu wa UNAMID ametumia mkutano huo kumpongeza Rais Omar Al Bashir wa Sudan kwa msamaha wake kwa waasi 259 waliokamatwa wakati wa mapigano ambapo kati yao hao wapo wapiganaji 66 waliokuwa wanasubiri adhabu ya kifo.

Amesema hatua hiyo inajenga kuaminiana kati ya pande kinzani huko Sudan.