Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Yemen yazidi kutwama- Baraza

Yemen yazidi kutwama- Baraza

Hali nchini Yemen inazidi kuwa mbaya na ya machungu huku raia wakilipa gharama ya mapigano yanayoendelea kwa miaka miwili sasa.

Rais wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Machi, Balozi Matthew Rycroft wa Uingereza amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari hii leo baada ya kikao cha faragha cha baraza hilo kilichoangazia Yemen.

Amesema hali hiyo ni dhahiri baada ya kusikiliza taarifa kutoka kwa mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Yemen Ismail Ould Cheikh Ahmed na kutoka kwa mwenyekiti wa kamati ya vikwazo dhidi ya Yemen, Balozi Koro Bessho.

Kwa mantiki hiyo amesema kushughulikia janga la kibinadamu inasalia changamoto wakati huu ambapo Yemen inakabiliwa na njaa kali, suluhu ya kisiasa ikisalia ndoto.

Alipoulizwa iwapo Bwana Ahmed ametaja mikakati mipya ya kusongesha upatikanaji suluhu hiyo, Balozi Rycroft amesema..

(Sauti ya Balozi Rycroft)

“Nadhani hakuna ukosefu wa mawazo na mapendekezo kuhusu mchakato wa amani Yemen. Kile kinachohitajika ni pande zote kuazimia kushiriki katika kutekeleza mawazo hayo. Nadhani anaweza kueleza mwenyewe lakini alikuwa anaelezea masuala ambayo amekuwa akiwasilisha hata siku za awali na ambazo pande husika zinapaswa kuzingatia. Lakini hakuonyesha matumaini ambayo huonyesha kila wakati.”