Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkakati mpya unalenga kusaidia zaidi waathirika wa ukatili wa kingono

Mkakati mpya unalenga kusaidia zaidi waathirika wa ukatili wa kingono

Umoja wa Mataifa umeweka bayana mkakati mpya wa kuzuia na kuchukua hatua dhidi ya vitendo vya ukatili wa kingono vinavyotekelezwa na wafanyakazi wake wanaotoa huduma mbali mbali duniani.

Mapendekezo hayo yamo kwenye ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres, ripoti ikielezwa kuwa inaangazia zaidi waathirika wa vitendo hivyo.

Katibu Mkuu aliwasilisha mapendekezo yake kupitia ujumbe wa video ambapo baadaye maafisa wa Umoja wa Mataifa akiwemo Nancee Bright kutoka ofisi ya mwakilishi maalum wa umoja huo kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo walizungumza na waandishi wa habari kueleza kwa kina yaliyomo kwenye ripoti hiyo ya kurasa 82.

Mathalani suala la kuwepo kwa mtetezi wa haki za wahanga wa ukatili wa kingono pamoja na kuanzishwa kwa wasaidizi wa Katibu Mkuu kwenye ofisi nne za ujumbe wa Umoja wa Mataifa ambako vitendo vya ukatili wa kingono vinaripotiwa zaidi.

(Sauti ya Nancee Bright)

"Kwa hiyo huyu mtetezi wa haki za wahanga atakuwa siyo tu anawasiliana na nchi ambamo kwayo ukatili huo umefanyika, bali pia na nchi ambako watuhumiwa wa vitendo hivyo wametoka. Mtetezi huyo pia atapatia wahanga taarifa kuhusu kinachoendelea kwasababu kwa sasa hivi jambo hilo halipo. Waathirika hawafahamu iwapo kuna kesi, na kama ipo ni lini inatajwa. Wahanga hawa hawafahamu kabisa kinachoendelea na hayo ndiyo mambo tunataka kubadili.”

Mkakati mwingine ni kuimarisha sera ya watoa taarifa na kulinda wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ambao wanaripoti visa vya ukatili wa kingono na unyanyasaji.