Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wajumuishwe ajenda 2030- Gilmore

Watoto wajumuishwe ajenda 2030- Gilmore

Naibu Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa, Kate Gilmore amesema mustakhbali bora wa dunia unawezekana iwapo masuala ya watoto yatapatiwa kipaumbele wakati wowote wa kujadili amani na maendeleo.

Amesema hayo wakati akifungua sehemu ya kwanza ya mkutano wa mwaka wa baraza hilo kuhusu haki za mtoto huko Geneva, Uswisi akisema hivi sasa takribani watoto milioni 70 wanaweza kufariki dunia kabla ya kufikisha umri wa miaka mitano.

Bi.Gilmore amesema hali ni mbaya zaidi kwa nchi za Afrika zilizo kusini mwa jangwa la Sahara ambako licha ya mafanikio kwingineko bado watoto na wajawazito wanafariki dunia kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika.

(Sauti ya Gilmore)

"Ajenda 2030 ya maendeleo endelevu ni ahadi baina ya vizazi ya kutokumuacha nyuma mtu yeyote, na watoto walioanchwa nyuma kabisa wanapaswa kufikiwa kwanza. Serikali na wadau wa maendeleo endelevu waongeze wigo wa ushiriki wa wadau na watoto wenyewe.”